Apr 09, 2020 02:40 UTC
  • Tishio la Marekani la kuikatia misaada WHO wakati huu wa corona

Baada ya kuenea sana maambukizi ya kirusi cha corona nchini Marekani na kupamba moto lawama dhidi ya utendaji mbovu wa rais wa nchi hiyo katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19, Donald Trump amekuwa akitapatapa huku na huko kwa kutoa tuhuma zisizo na msingi. Huko nyuma aliilaumu China kuwa imechelewa kuijulisha Marekani kuhusu ugonjwa huo na sasa amelivurumishia Shirika la Afya Duniani WHO tuhuma hizo hizo na kutishia kulikatia misaada.

Kitendo cha serikali ya Donald Trump cha kushindwa kutoa taarifa haraka na kutochukua hatua mwafaka za kuzuia kuenea corona pamoja na misimamo tofauti ya kukinzana iliyochukuliwa na rais huyo mwanagenzi wa Marekani kuhusu COVID-19, kumepelekea kuzuka lawama na mashinikio mengi dhidi yake. Sasa ili kujipunguzia mashinikizo, Trump kwa mara nyingine amerudia hila zake za kila siku, za kuzusha mijadala mipya, alianza na China sasa amelivamia Shirika la Afya Duniani WHO na kulishambulia shirika hilo kwa kile alichokiita ni kuipendelea China ikiwa ni njia ya kumshinikiza mkuu wa shirika hilo ajiuzulu.

Trump na wakuu wa ngazi za juu wa serikali yake wamefanya njama za kujaribu kuonesha kuwa ugonjwa wa COVID-19 asili yake ni China na imefikia hadi Trump ameuita ugonjwa huo kwa jina la kirusi cha China. Hata hivyo Beijing ilifanikiwa kukigundua kirusi hicho mwanzoni kabisa mwa kuenea kwake na kutoa tahadhari kuhusu hatari zake. Lakini viongozi wa Marekani wanadai kuwa idadi ya vifo na maambukizi iliyotangazwa na China si sahihi, ikiwa ni katika njama zao nyingine za kuichafulia jina China na kujipunguzia mashinikizo yao ya ndani ya Marekani. Hata hivyo hivi karibuni msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alijibu madai hayo ya viongozi wa White House wanaodai kuwa corona imeanzia Wuhan, China, na kusema kuwa, madai hayo ya Washington hayana maadili wala si ya watu wanaojali majukumu yao.

Maafa ya corona mini New York, Marekani

 

Hivi sasa hali imezidi kuwa mbaya nchini Marekani. Viongozi wa White House hasa Trump mwenyewe wanatafuta kondoo wa kumtoa kafara na inaonekana Shirika la Afya Duniani (WHO) ndilo windo rahisi kwao kwa hivi sasa. Mbali na China, viongozi wa Washington wanaituhumu WHO kuwa eti ndiyo sababu ya kuenea sana ugonjwa wa corona huko Marekani ili kujipunguzia mashinikizo na kuzipotosha fikra za walio wengi nchini Marekani. Lakini wanaomkosoa Trump wanasema kuwa, si tu rais huyo amefanya uzembe mkubwa ndani ya Marekani wa kushindwa kutangaza haraka maambukizi ya corona na kutokuwa na stratijia na mkakati wowote wa kukabiliana na ugonjwa huo na hakufanya haraka kuingiza vifaa vya kukabiliana na COVID-19, lakini pia amefanya makosa katika siasa za nje. Mmoja wa wakosoaji hao ni Seneta Chris Murphy ambaye anasema, kwa miaka mingi nyuma, Marekani ilikuwa na mpango wa "Predict" ambao ulikuwa ukiisaidia nchi hiyo kugundua virusi hatari duniani na kuzuia kuenea ndani ya Marekani, lakini Trump alifuta mpango huo miezi miwili kabla ya kugunduliwa corona mjini Wuhan, China. 

Kwa kweli mara zote Trump ameonesha kuwa hana kifua cha kuvumilia lawama na ukosoaji. Vile vile amekuja na siasa za kupinga ushirikiano wa kimataifa; siasa za Marekani kujikumbizia kila kitu upande wake bila ya kujali maslahi ya wengine. Huko nyuma Marekani ilijitoa kwenye mikataba mbalimbali ya kimataifa na sasa Trump anatishia kulikatia misaada Shirika la Afya Duniani (WHO) na kumshinikiza mkuu wa shirika hilo ajiuzulu.

Maafa ya COVID-19 nchini Italia na bado rais wa Marekani anatishia kuvuruga jitihada za kimataifa zakupambana na corona

 

Katika ukurasa wake wa Twitter, Trump ameandika: Shirika la Afya Duniani limefanya kosa kubwa. Marekani inatoa mchango mkubwa wa kifedha kwa shirika hilo kutokana na sababu zake maalumu, lakini katika upande wa pili, shirika hilo linaipendelea sana China. Tutalichunguza kwa kina jambo hilo.

Marekani imeanzisha vita dhidi ya WHO katika hali ambayo dunia hivi sasa imegubikwa na janga la corona na hivi sasa ulimwengu unahitajia mno ushirikiano na mshikamano katika masuala ya tiba na matibabu kuliko wakati mwingine wowote.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom amesema: Ushirikiano wa dunia nzima katika kukabiliana na corona, ni jambo la dharura.

Maelfu ya watu wameshapoteza maisha hadi hivi sasa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 duniani, lakini Trump na serikali yake ndio kwanza wanaanzisha migogoro mipya duniani badala ya kutuliza hali ya mambo na kuzifanya fikra zote za walimwengu zielekezwe kwenye kuudhibiti na kuushinda ugonjwa huo hatari.

Tags

Maoni