Apr 09, 2020 02:41 UTC
  • Virusi vya Corona vyasababisha hasara ya dola bilioni moja katika utajiri wa Trump

Gazeti la The Guardian limeeleza kuwa utajiri wa Rais Donald Trump wa Marekani, umepata hasara ya dola bilioni moja kutokana na kuenea virusi vya Corona.

Gazeti hilo limeashiria maambukizi makubwa ya virusi vya Corona nchini Marekani na karantini iliyotangazwa nchini humo na kufafanua kuwa, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Trump amepoteza sehemu kubwa ya utajiri wake kutokana na karantini iliyosababishwa na Corona. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mtandao wa Forbes unaochapisha orodha ya mabilionea wa mwaka umeandika kuwa, utajiri wa Trump ulishuka kutoka dola bilioni tatu na milioni 100 tarehe mosi mwezi Machi na kufikia dola bilioni moja na milioni 200 tarehe 18 mwezi Machi kutokana na hofu iliyoyakumba masoko ya hisa kutokana na kuenea kwa virusi vya Corona.

Corona, pigo kubwa linalomwandama Trump

Ripoti ya 34 ya kila mwaka ya jarida la Forbes ambayo ndani yake kumetajwa majina ya matajiri wakubwa duniani imesema kuwa, kuporomoka masoko ya hisa kunakotokana na virusi vya Corona duniani, kumewafanya matajiri 267 duniani kupoteza utajiri wao wa mabilioni ya dola. Aidha ripoti zinaarifu kwamba, Rais Donald Trump wa Marekani amefunga maeneo 17 yanayomuingizia fedha katika maeneo tofauti ya dunia sambamba na kuwafuta kazi karibu watumishi 1,500 au kuwalazimisha wengine kwenda likizo ya lazima.

Tags

Maoni