Apr 09, 2020 11:19 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN asisitiza kuiunga mkono WHO baada ya matamshi ya Trump

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Shirika la Afya Duniani, WHO, ambalo ni taasisi ya umoja huo, linapasa kuungwa mkono duniani kote, akisema kuwa chombo hicho kimekuwa muhimu sana kikichukua msimamo wa kimataifa kukabiliana na mlipuko wa janga la ugonjwa wa COVID-19 au corona.

Katika taarifa yake aliyoitoa kupitia msemaji wake jijini New York, Guterres amesema, “janga la COVID-19 ni moja ya changamoto hatari zaidi ambazo dunia hii imewahi kukabiliana nazo. Na zaidi ya yote ni janga kubwa la kibinadamu lenye madhara kijamii na kiuchumi.”

Gutteres ametoa tamko hilo baada ya  Rais Donald Trump wa Marekani kulituhumu Shirika la Afya Duniani kuwa linaipendelea China. Katika ukurasa wake wa Twitter, Trump ameandika: "Shirika la Afya Duniani limefanya kosa kubwa. Marekani inatoa mchango mkubwa wa kifedha kwa shirika hilo kutokana na sababu zake maalumu, lakini katika upande wa pili, shirika hilo linaipendelea sana China. Tutalichunguza kwa kina jambo hilo."

Kufuatia matamshi hayo, Gutteres amesema maelfu ya wafanyakazi wa WHO wako mashinani wanapambana na corona mstari wa mbele, wakisaidia nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na kuhudumia watu walio hatarini zaidi huku wakiwapatia mwongozo, mafunzo, vifaa na hata misaada ya kuokoa maisha.

 

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus

 

Mapema akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video mjini Geneva, Uswisi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus ametaka watu waache kuingiza siasa kwenye suala la ugonjwa wa COVID-19.

Amesema: "Sijali nani anasema nini kunihusu."  Aidha ametoa wito kwa wote kujikita katika kuokoa maisha, akisema hakuna muda wa kupoteza.

 

Tags

Maoni