Apr 10, 2020 02:32 UTC
  • Indhari ya WTO ya kutokea mgogoro mkubwa zaidi wa kiuchumi katika historia ya mwanadamu

Mlipuko wa virusi vya Corona na maradhi ya Covid-19 kwa sasa umeenea karibu katika mataifa yote ya ulimwengu.

Filihali ulimwengu unakabiliwa na tukio ambalo halikutabiriwa ambalo limekuwa na taathira hasi kwa mwenendo wa uchumi ambao mustakabali wake unakabiliwa na giza totoro. Hali hii imepelekea kutolewa indhari mbalimbali. Roberto Azevedo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) alitahadharisha Jumatano ya juzi tarehe 8 Aprili kwamba, kuenea ulimwenguni kote virusi vya Corona yumkini kukapelekea kuibuka mgogoro mkubwa zaidi wa kiuchumi ambao haujawi kushuhudiwa katika historia ya mwanadamu.

Shirika la Biashara Duniani (WTO) limetangaza katika takwimu zake za hivi karibuni kabisa kwamba, kuenea virusi vya Corona kutapelekea kupungua kwa asilimia 13 hadi 23  ya mabadilishano ya kibiasahara katika mwaka huu wa 2020. Ripoti ya shirika hilo inaeleza kwamba, kuporomoka kwa masoko ya fedha katika mwaka huu kutakuwa kukubwa zaidi ya mgogoroi wa kiuchumi ulioikabili dunia mwaka 2008

Roberto Azevedo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO)

 

Kadhalika Shirika la Biashara Duniani (WTO) limetabiri kwamba, biashara ya dunia ambayo kabla ya virusi vya Corona ilikuwa imeathiriwa na mivutano ya kibiashara pamoja na hali tata na isiyoeleweka kutokana na kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya (Brexit), mwaka huu itakabiliwa na mporomoko zaidi katika pembe zote za dunia.

Roberto Azevedo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) aidha amesema kuwa, janga la Corona kabla ya chochote ni balaa la kiafya ambapo mataifa ya dunia yanalazimika kuchukua hatua ambazo hazijawahi kushuhudiwa kwa ajili ya kulinda maisha ya raia wao. Kupungua kusikozuilika kwa biashara na uzalishaji ni matokeo machungu ambayo yatazikumba familia na shughuli katika sekta mbalimbali.

Indhari ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) kuhusiana na matokeo angamizi kwa uchumi na biashara kutokana na kuenea virusi vya Corona kimsingi inabainisha wasiwasi mkubwa wa taathira ya virusi hivi ambavyo havijawahi kushuhudiwa katika historia ya mwanadamu ambavyo vimeibuka ghafla na bila kutarajiwa na hivyo kuleta mshtuko mkubwa kwa ulimwengu mzima.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa analizungumia janga la virusi vya Corona kwa kusema: Virusi hivi vimelenga misingi ya jamii, na kuibuka kwa virusi hivi ni changamoto kubwa zaidi kwa jamii ya mwanadamu tangu kuanzishwa Umoja wa Mataifa kufuatia Vita vya Pili vya Dunia.

 

Kuenea virusi hivi duniani kote na mamilioni ya watu kulazimika kuwa karantini, kumeufanya uchumi wa dunia ukaribie kusambaratika. Kwa kuzingatia kuwa, madola ya Ulaya na Marekani ndio mataifa yaliyoathiriwa zaidi na virusi vya Corona, tayari kunashuhudiwa taathira haribifu za maradhi haya ya Covid-19 katika mataifa hayo, ambapo mdodoro wa uchumi ambao haujawahi kushuhudiwa unazidi kuongezeka.

Kwa sasa Marekani na mataifa ya Ulaya yanakabiliwa na mgogoro mkubwa katika uga wa kiuchumi na kibiashara ambapo sekta ya viwanda na ile ya utoaji huduma kama usafiri na uchukuzi au utalii zinaonekana kuathiriwa vibaya zaidi ikilinganishwa na sekta nyingine. Miongoni mwa matokeo mabaya ya hali hii ni kuongezeka mno ukosefu wa ajira na kupungua pakubwa ustawi wa uchumi katika madola ya Magharibi na vile vile kwa nchi ambazo zina uhusiano wa karibu wa kisiasa, kiuchumi na kibiashara na ulimwengu wa Magharibi.

Shirika la Ndege la Emirates ni miongoni mwa mashirika makubwa ya ndege yanayoendelea kupata hasara kutokana na kusitisha safari zake nyingi za abiria za kimataifa kufuatia virusi vya Corona

 

Akthari ya weledi na wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kwa kuzingatia taathira hasi za Corona kwa uchumi wa dunia hususan kwa kundi la G20, hata baada ya kuvuka kipindi hiki cha virusi vya Corona, uchumi wa mataifa na mfumo wa kiuchumi na kibiashara kimataifa utakumbwa na mabadiliko makubwa ambapo kuanzia sasa ishara zake zimeanza kujitokeza. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, wataalamu wa masuala ya afya wameshatahadharisha kwamba, virusi vya Corona vitabakia kwa muda mrefu na kugeuka kuwa jinamizi baya zaidi kwa walimwengu.

Wataalamu wengi wa masuala ya kiuchumi wanatabiri kuwa, kutokana na kuwa, kudhibiti na kutokomeza virusi vya Corona kunahitajia kupungua maingiliano na mchanganyiko usio wa dharura wa wanadamu ili kukata mnyororo wa virusi hivyo jambo ambalo nalo litapelekea kupungua kwa harakati nyingi za kiuchumi, hivyo basi suala la uchumi kudorora ni kitu ambacho hakiepukikii na litakuwa jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa. Tayari ishara za hilo zimeshajitokeza huko Marekani na katika mataifa ya Ulaya na kwa mataifa mengine makubwa kiuchumi yanayosafirisha bidhaa kwa wingi kama China na India ambayo kwa sasa yanapitia kipindi cha kukabiliwa na upungufu mkubwa wa oda za bidhaa.

Tags

Maoni