Apr 10, 2020 02:33 UTC
  • Giuseppe Conte
    Giuseppe Conte

Waziri Mkuu wa Italia ameonya kuhusu hatari ya kusambaratika Umoja wa Ulaya (EU) baada ya mgogoro wa corona kutokana na utendaji dhaifu sana wa umoja huo.

Giuseppe Conte ametoa onyo hilo kali katika mazungumzo na gazeti la Bild la nchini Ujerumani na kuulaumu umoja huo kwa kushindwa kuisaidia Italia wakati huu wa mgogoro wa corona akisisitiza kuwa, kama Ulaya itadumaa, basi kuweko nchi kama Ujerumani hakutakuwa na maana yoyote.

Vile vile Waziri Mkuu huyo wa Italia amesema, si jambo rahisi kwa nchi yake kurejea kama ilivyokuwa kabla ya mgogoro wa corona. Italia ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu waliopoteza maisha kwa ugonjwa wa COVID-19, na kwa upande wa idadi kubwa ya watu walioambukizwa ugonjwa huo hatari, ni ya tatu baada ya Marekani na Uhispania.

Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya (EU) mjini Brussels, Ubelgiji

 

Huku hayo yakiripotiwa, hatimaye Umoja wa Ulaya umepasisha Euro bilioni 20 za kupambana na maambukizi ya kirusi cha corona.Shirika la habari la IRNA limemnukuu Joseph Barrel, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya akisema jana kwamba, fedha hizo zimetengwa kwa jina la timu ya Ulaya ya kuzisaidia nchi jirani za umoja huo zilizoathiriwa na corona na vile vile ni kwa ajili ya kuzisaidia nchi za eneo la Caucasia, Ulaya Mashariki, Asia Magharibi, Asia na Pasifiki, Afrika, Amerika ya Latini na visiwa vya Caraib ili kuzuia maambukizi ya kirusi hicho na athari zake mbaya.

Ikumbukwe kuwa, Brussels, mji mkuu wa Ubelgiji, ndiyo makao makuu ya Umoja wa Ulaya (EU). Ukitoa Marekani, nchi za Ulaya za Uhispania, Italia, Ujerumani na Ufaransa ndizo zinazoongoza kwa maambukizi makubwa zaidi ya corona duniani.

Tags

Maoni