Apr 10, 2020 08:22 UTC
  • Guterres atahadharisha kuhusu hujuma ya silaha ya kibiolojia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kufanyika hujuma na mashambulizi ya silaha za kibiolojia katika kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona duniani.

Antonio Guterres ambaye jana jioni alihutubia kikao cha  Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video alisema kuwa, mlipuko wa virusi vya corona ni tishio kwa usalama na amani ya kimataifa. 

Amesema kuwa, udhaifu na madhara yanayosababishwa na ugonjwa wa kuambukiza wa virusi vya corona yanaweza kuwa dirisha la hujuma na mashambulizi ya kigaidi ya silaha za kibiolojia na kwamba yumkini makundi ya kigaidi yakafanya mashambulizi kwa kutumia silaha hiyo katika kipindi hiki ambapo nchi mbalimbali zimejikita katika mapambano na virusi hivyo. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, virusi hivi vinaweza kusababisha mgogoro mkubwa wa kiuchumi duniani hususan kwa jamii tete katika nchi zinazostawi. 

Zaidi ya watu 1,605,683 wameambukizwa virusi vya corona kote dunia na 95,765 miongoni mwao wameaga dunia. 

Tags

Maoni