Apr 14, 2020 12:33 UTC
  • Indhari ya UN baada ya Saudia kuwafukuza nchini humo raia wa Ethiopia

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, hatua ya watawala wa Riyadh ya kuwatimua nchini Saudi Arabia wafanyakazi wahajiri raia wa Ethiopia itasababisha kuenea na kusambaa virusi vya Corona.

Catherine Sozi, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Ethiopia amesema, "wimbi kubwa la kuwafurusha wahamiaji ambalo halikuwa limepangwa litaongeza kasi ya kusambaa kwa virusi hivyo. Tunaiomba Saudia isimamishe kwa muda hatua hiyo ya kuwatimua wahajiri."

Waraka wa Umoja wa Mataifa umefichua kuwa, Saudia inapanga kuwafukuza nchini humo Waethiopia wapatao laki mbili, huku Shirika la Uhamiaji la umoja huo likisema, hadi sasa Wahabeshi 2,870 wamefukuzwa Saudia tangu kuanza kwa janga la Corona. 

Serikali ya Ethiopia imeghadhabishwa pia na kuonyesha wasi wasi wake kufuatia hatua hiyo ya Saudia ya kuwatimua raia wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika bila ya kuwafanyia vipimo vya Corona.

Wahajiri raia wa Ethiopia nchini Saudia

Utawala wa Riyadh unadai kuwa wageni hao wanaondoka nchini humo kwa ridhaa yao na baada ya kufuata taratibu za kisheria.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali ya Ethiopia, hadi sasa watu 71 wameathirika na virusi vya Corona ambapo kati yao watu 10 wamepoteza maisha.

Tags

Maoni