Apr 15, 2020 08:14 UTC
  • UN yakerwa na hatua ya Trump kuikatia ufadhili WHO wakati huu wa Corona

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitizia udharura wa kuungwa mkono Shirika la Afya Duniani (WHO), muda mfupi baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa nchi hiyo imelikatia misaada yake ya kifedha shirika hilo.

Antonio Guterres amesema katika taarifa kuwa, "ninaamini kuwa, Shirika la Afya Duniani lazima liungwe mkono kwa kuwa lina umuhimu mkubwa katika jitihada za dunia za kushinda vita dhidi ya Covid-19." 

Jana Jumanne, Trump alitangaza kuwa Washington imeikatia misaada yake ya kifedha WHO, kwa madai kuwa shirika hilo linalishughulikia visivyo janga la Corona.

Alidai kuwa taasisi hiyo ya kimataifa ya afya Disemba mwaka jana ilikataa kujibu au kutoa 'taarifa muhimu' iliyoashiria kuwa virusi vya Corona vinaweza kuenezwa kupitia wanadamu.

Trump amekuwa akilituhumuu Shirika la Afya Duniani kwamba linaipendelea China na eti lilichelewa kutangaza hatari ya kuenea virusi vya Corona duniani.

Tedros Adhanom, Katibu Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)

Tedros Adhanom, Katibu Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amekuwa akikosoa vikali mienendo na tuhuma za Trump dhidi ya shirika hilo, akisitiza kuwa huu sio wakati wa kuzozana na kutuhumiana, bali ni huu ni wakati ambao nchi zote za dunia zinapaswa kushirikiana na kuungana iwapo zinataka kulitokomeza janga la Corona.

Mwaka jana Marekani iliipa WHO msaada wa dola milioni 400, ambayo ni asilimia 15 ya bajeti ya shirika hilo la afya lenya makao makuu yake mjini Geneva, Uswisi.

Tags

Maoni