Apr 18, 2020 00:42 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Mgogoro wa kiuchumi unaosababishwa na Corona unatishia uhai wa mamia ya maelfu ya watoto

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, yumkini mwaka huu wa 2020 ukashuhudia mamia ya maefu ya watoto wakiaga dunia kutokana na mgogoro wa kiuchumi ambao chimbuko lake ni kuenea virusi vya Corona kote ulimwenguni.

Umoja wa Mataifa umeashiria katika ripoti yake hiyo matatizo ya kimaisha yanayozikabili familia mbalimbali kutokana na mgogoro wa kiuchumi uliosababishwa na virusi vya Corona na kueleza kwamba, huenda mamia ya maelfu ya watoto wakapoteza maisha mwaka huu.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, matokeo ya virusi vya Corona ulimwenguni ni kushadidi umasikini ambapo makumi ya mamilioni ya watu wataongezeka kwenye idadi ya watu masikini ulimwenguni.

Takwimu za mwaka uliopita wa 2019 zinaonyesha kuwa, takribani watoto milioni 386 walikuwa katika umasikini wa kupindukia na hivi sasa yumkini watoto wengine milioni 42 hadi 66 wakaongezeka katika idadi hiyo ikiwa ni natija ya athari mbaya za virusi vya Corona.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

 

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema kuwa, hivi sasa tunapaswa kukabilianan na vitisho vinavyowakabili watoto, tuchukue hatua katika uwanja huo; na viongozi wa dunia wanapaswa kufanya kila wawezalo kwa ajili ya kupunguza makali yanayosababishwa na virusi vya Corona.

Shirika la Biashara Duniani (WTO) limetangaza katika takwimu zake za hivi karibuni kabisa kwamba, kuenea virusi vya Corona kutapelekea kupungua kwa asilimia 13 hadi 23  ya mabadilishano ya kibiasahara katika mwaka huu wa 2020.

Tags

Maoni