Apr 30, 2020 08:01 UTC
  • UN: Jeshi la Myanmar linaendelea kuwafanyia jinai Waislamu Warohingya

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Myanmar amelituhumu jeshi la nchi hiyo kuwa lingali linawatendea jinai za kivita na zilizo dhidi ya binadamu Waislamu wa jamii ya Rohingya katika majimbo mawili ya nchi.

Yanghee Lee alisema hayo jana Jumatano katika taarifa aliyotoa mwishoni mwa muhula wake wa kuhudumu kama  Ripota Maalumu wa UN nchini Myanmar na kueleza bayana kuwa, "katika hali ambayo dunia imetingwa na janga la Covid-19, jeshi la Myanmar linaendelea kushadidisha hujuma zake katika jimbo la Rakhine, likiwalenga raia."

Amesema Jeshi la Myanmar linalofahamika kama Tatmadaw linaendelea kuzisababisha maumivu na machungu jamii zinazoishi katika majimbo ya Rakhine na  Chin na kwamba "linakanyaga kwa mpangilio maalumu kanuni za msingi za sheria za kimataifa za utu na haki za kibinadamu." 

Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayeondoka ameongeza kuwa, mienendo ya wanajeshi wa Myanmar dhidi ya jamii ya Waislamu wa Rohingya katika majimbo ya Rakhine na Chin yumkini ni jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.

Yanghee Lee, Ripota Maalumu wa UN anayeondoka

Itakumbukwa kuwa wimbi jipya la mauaji, mashambulizi na ubakaji wa jeshi la Myanmar katika mkoa wa Rakhine kuwalenga Waislamu wa Rohingya, lilianza tarehe 25 Agosti mwaka 2017 ambapo zaidi ya Waislamu elfu sita waliuawa na wengine elfu nane kujeruhiwa.

Aidha zaidi ya Waislamu wengine milioni moja wa jamii hiyo walilazimika kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh wakitoroka ukatili huo wa jeshi la Mynamar likishirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada.

Tags

Maoni