May 17, 2020 12:21 UTC
  • Onyo la Steven Mnuchin juu ya uwezekano wa kusambaratika uchumi wa Marekani

Kuenea kwa virusi vya Corona nchini Marekani kumeisababishia jamii ya nchi hiyo matatizo makubwa ya kila upande hususan kwenye upande wa uchumi.

Katika uga wa uchumi, hivi sasa Marekani inakabiliwa na mgogoro mkubwa pamoja na mdororo wa uchumi ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya nchi hiyo. Aidha viwango vya ukosefu wa ajira, kufungwa vituo vya ajira, kupungua kwa shughuli za mashirika na viwanda n.k, ni mambo ambayo yameendelea kuisababishia hasara kubwa ya kiuchumi Marekani katika historia yake. Suala hilo ndilo limemfanya Steven Mnuchin, Waziri wa Fedha wa Marekani kutoa onyo kali. Jumatano iliyopita na kutokana na madhara makubwa ambayo huwenda yakaupata uchumi wa nchi hiyo kutokana na virusi vya Corona, Mnuchin alisema: "Iwapo Washington itaendelea kusubiri kwa muda mrefu kufunguliwa shughuli za uchumi kutokana na virusi vya Corona, basi uchumi wa nchi hii utakumbwa na hatari ya kusambaratika." Waziri wa fedha wa Marekani alitabiri kwamba katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ya mwaka huu nchi hiyo itakumbwa na 'hali mbaya' katika uga wa kiuchumi. Pamoja na hayo alidai kwamba iwapo uchumi wa nchi hiyo utafunguliwa kwa umakini, basi hali itawezekana kurekebishika. Steven Mnuchin anaamini kwamba kusubiri kwa muda mrefu hadi kuondoka virusi vya Corona, kunaweza kusababisha hatari ya kusambaratika uchumi na kuathiri usalama na sekta ya afya.

Serikali ya Trump iliyofeli kukabiliana na virusi vya Corona

Serikali ya Trump inadai kwamba sekta ya uchumi inahitaji msukumo mkubwa wa kifedha, na ili kufanikisha jambo hilo itatenga kiwango kikubwa cha fedha. Licha ya hatua za serikali ya Trump, akthari ya viongozi wa ngazi ya juu katika serikali na katika ngazi ya majimbo ya nchi hiyo, wanapinga suala la kufunguliwa mapema na kuanzishwa shughuli za kiuchumi bila ya utaratibu na kwamba jambo hilo litapelekea kuibuka wimbi la pili la maambukizi ya virusi vya Corona nchini humo. Anthony Fauci, Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa ya kuambukiza nchini Marekani na mjumbe wa jopo la kupambana na Corona katika ikulu ya White House, ameonya kuhusu kufunguliwa mapema shughuli za kiuchumi nchini humo. Kwa kuzingatia kwamba Marekani ndiyo muathirika mkubwa zaidi duniani wa maambukizi na vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa wa Covid-19, hivi sasa inatarajia kuongezeka zaidi vifo vinavyotokana na maradhi hayo. Kwa mujibu wa Christopher Murray, Mkuu wa Taasisi ya Takwimu na Uchunguzi wa Afya katika Chuo Kikuu cha Washington, idadi ya watakaofariki wa virusi vya Corona nchini Marekani huwenda ikafikia watu laki moja na elfu 47 hadi kufikia tarehe 4 Agosti mwaka huu. Hii ni katika hali ambayo wasi wasi zaidi kuhusu kuibuka kwa wimbi la pili vya virusi vya Corona nchini humo, umezidi kuongezeka. Mkabala wake Rais Donald Trump ameonyesha kushangazwa na indhari ya Anthony Fauci kuhusu kufunguliwa mapema shughuli za kiuchumi nchini Marekani. Hii ni katika hali ambayo wakosoaji wanaamini kwamba lengo hasa la Trump na la viongozi wa ngazi ya juu wa serikali la kusisitiza kufunguliwa haraka shughuli za kiuchumi, linahusiana na masuala ya uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka huu.

Ndoto inayofifia ya Trump ya kuifanya Marekani kuwa ya kibeberu zaidi

Ni ukweli na ni dhahiri kwamba Trump na washauri wake wameshindwa kukabiliana na virusi vya Corona na hivyo wamegeuza mwelekeo kwa kusisitiza kufunguliwa haraka shughuli za kiuchumi. Wanatetea mabadiliko yao hayo wanayotaka yafanyike kwa kudai kwamba lengo lake ni kuzuia kusambaratika zaidi uchumi wa Marekani na kujiandaa kukabiliana na Corona katika msimu wa vuli mwaka huu. Kimsingi hatua ya Marekani ya kutaka kufunguliwa upesi shughuli za kiuchumi, ni sawa na kuwasukuma raia wa nchi hiyo kwenye lindi la kifo. Kama alivyosema Nancy Pelosi, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani ambaye sambamba na kukosoa usimamizi mbovu wa serikali ya Trump katika uga wa kukabiliana na Corona amesisitiza kwamba badala ya Trump kuwaeleza uongo raia ni lazima aweke wazi juu ya mgogoro wa Corona ndani ya Marekani na kisha achukue maamuzi kwa msingi huo. Hivi sasa sambamba na Marekani kukabiliwa na mgogoro na mdororo wa uchumi, inaandamwa pia na matatizo kadha wa kadha ambayo hayakuwahi kushuhudiwa hapo kabla isipokuwa wakati wa mgogoro wa kiuchumi wa mwaka 1929. Matatizo hayo ni pamoja na baa la njaa, kupangwa foleni zenye urefu wa kilometa kadhaa kwa ajili ya kupokea msaada wa chakula, kuongezeka umasikini na kukosa makazi, kurundikana madeni yaliyoyaelemea matabaka ya kati na ya watu masikini na kushindwa kulipa madeni hayo, na matokeo yake yakawa ni watu kupoteza nyumba zao na suhula za maisha na kuongezeka malalamiko ya kijamii ya kufikia hadi hata kutumia silaha za moto na hivyo kutoweka usalama wa kijamii ndani ya nchi hiyo.

Tags