May 19, 2020 07:39 UTC
  • Trump atishia kujiondoa WHO, asema shirika hilo ni kikaragosi cha China

Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kuiondoa Marekani kwenye Shirika la Afya Duniani WHO, akidai kuwa taasisi hiyo ya kimataifa ni kikaragosi cha China.

Trump ametoa vitisho hivyo katika barua aliyomuandikia Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Dunia, Tedros Adhanom Gabrayesus ambapo amesema, "Marekani itaikatia misaada WHO kikamilifu iwapo haitapiga hatua kubwa za kujiboresha ndani ya siku 30 zijazo."

Rais huyo wa Marekani ametuma ujumbe uliouambatanisha na nakala ya barua hiyo kwenye ukurasa wake wa Twitter na kuandika: Tunaipa WHO dola milioni 450 kila mwaka, lakini hawatutendei wema, wamekuwa wakitupa ushauri mbaya.

Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita wa Aprili, Trump alitoa tuhuma kali na za kichochezi dhidi ya shirika hilo akidai kwamba linaipendelea China, na hivyo akachukua uamuzi wa kulitakia misaada ya kifedha.

Mbali na kuilaumu WHO, Trump pia amekuwa akidai kwamba China haikuweza kutoa kwa wakati muafaka taarifa za kuenea virusi vya corona wala kukabidhi takwimu sahihi za virusi hivyo kwa Shirika la Afya Duniani; ambapo pia alitishia kuwa huenda akaamua kukata uhusiano wa Washington na Beijing.

US, muathirika mkubwa zaidi wa corona duniani kutokana na uzembe wa utawala wa Trump

Hata hivyo wakosoaji na wapinzani wake wanasema lengo la Rais huyo wa Marekani la kuielekezea WHO na China kidole cha lawama kwa janga la corona ni kujaribu kupotosha fikra za walio wengi na kuficha uzembe wa serikali yake ulioifanya Marekani iwe muathirika mkubwa zaidi wa mlipuko wa corona duniani.

Hadi sasa zaidi ya Wamarekani zaidi ya milioni moja na laki tano wameambukizwa virusi vya corona, huku wengine zaidi ya 90,000 wakiaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini humo.

 

Tags

Maoni