May 20, 2020 06:52 UTC
  • Matamshi ya Rais wa Marekani kuhusu kufaidika Taliban na uwepo wa askari wa Marekani nchini humo

Rais wa Marekani amesema uwepo wa askari wa nchi yake huko Afghanistan ni kwa faida ya Taliban na hivyo kundi hilo halitaki askari wa Marekani waondoke.

Donald Trump ameandika ujumbe katika ukurasa wake binafsi wa Twitter na kudai kuwa, wanajeshi  wa Marekani nchini Afghanistan wamekuwa na nafasi ya polisi tu.

Matamshi ya Trump kuwa uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan ni kwa maslahi ya kundi la Taliban ni kukiri ukweli kuwa, uwepo wa askari hao vamizi ni chanzo cha kuimarika makundi ya kigaidi na yenye kufurutu ada katika eneo.

Afghanistan ni sehemu ya eneo la kijiografia lenye umuhimu mkubwa wa kistratijia na katika miaka ya hivi karibuni imekuwa medani ya kushadidi harakati za makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu ada.

Kutokana na stratijia ya Marekani, hata eneo la kaskazini mwa Afghanistan ambalo katika miaka ya kwanza ya karne ya 21 lilikuwa na amani na utulivu, katika miaka ya hivi karibini limeshuhudia ukosefu mkubwa wa usalama. Katika eneo hilo la Afghanistan, makundi mbali mbali ya magaidi wakufurishaji kuanzia kundi la ISISI au Daesh hadi makundi yenye misimamo mikali yamekuwa yakipata himaya ya Marekani kwa lengo la kutoa pigo kwa Russia na China.

Umoja wa Mataifa unasema kushadidi hujuma za kigaidi nchini Afghanistan kumeathiri vibaya hali ya mambo nchini humo. Leo makundi ya kigaidi yameeneza harakati zao katika karibu maeneo yote ya nchi hiyo. Kutokana na uwepo wa wanajeshi vamizi wa nchi za Magharibi huko Afghanistan, leo makundi ya kigaidi yameweza kupata vyanzo vya pesa na silaha na hivyo kuimarika sana. Mbali na kuenea ugaidi baada ya kuingia wanajeshi vamizi wa kigeni nchini Afghanistan, hivi sasa pia biashara haramu ya dawa za kulevya imeimarika na ni chanzo kikuu cha fedha kwa makundi ya kigaidi.

Hali baada ya hujuma ya kigaidi Afghanistan

Mwaka 2001 kabla ya kuingia wanajeshi vamizi nchini Afghanistan, ukulima wa mihadarati aina ya afyuni ulikuwa ni tarkibani tani 200 kwa mwaka lakini kufikia mwaka 2019 kiwango hicho kilikuwa kimefika tani 2000 na hilo limejiri chini ya uangalizi wa wanajeshi vamizi wanaoongozwa na Marekani. Taarifa za siri zinadokeza kuwa kiwango kikubwa cha faida zinazotokana na uzalishaji na uuzaji wa dawa za kulevya nchini Afghanistan huingia kwenye mifuko ya wanajeshi vamizi wanaoongozwa na Marekani na pia ni chanzo kikuu cha fedha kwa makundi ya kigaidi.

Omar Nasser, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema Marekani na makundi ya kigaidi nchini Afghanistan hupata faida ya mabilioni ya dola kila mwaka kutokana na biashara haramu ya dawa za kulevya. Wanajeshi wa Marekani wako katika maeneo ya mashamba ya madawa ya kulevya nchini Afghanistan na hawachukui hatua yoyote kuzuia ukulima huo kwa sababu wanapata faida ya mabilioni ya dola kutokana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini humo.

Kwa hakika tunapaswa kusema kuwa, wanajeshi wa Marekani na makundi ya kigaidi na yenye misimamo mikali yanasaidia na kuimarishana na sasa ni upanga wenye ncha mbili wa biashara ya dawa za kulevya ambayo inaharibu mustakabli wa Afghanistan.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Trump amesema wanajeshi wa Marekani ni kama polisi ya Afghanistan  ingawa matamshi hayo yanaonyesha pia kushindwa katika medani na kurudi nyuma kutoka ahadi za watawala wa Washington, lakini katika upande mwingine matamshi hayo yanaonyesha kuwa Marekani imefumbia macho ugaidi katika nchi hiyo.

Aidha tunapaswa kuuliza iwapo Marekani kama inavyodai sasa nafasi yake ni ya kipolisi tu nchini Afghanistan basi ni kwa nini katika wiki za hivi karibuni imechukua misimamo ya kuunga mkono makundi ya kigaidi na misimamo mikali na inaishinikiza serikali ya Afghanistan itekeleza matakwa ya kujitakia makuu ya makundi hayo?

Wanajeshi vamizi wa Marekani wakiwa katika shamba la mihadarati aina ya afyuni nchini  Afghanistan

Ghadhabu ya siku za hivi karibuni ya wakuu wa Afghanistan baada ya Marekani kuwaondoa hatiani magaidi wa Taliban ambao wanalaumiwa kuhusika na hujuma dhidi ya hospitali ya wanawake na watoto mjini Kabul ni ishara nyingine ya ushirikiano wa karibu wa Marekani na makundi yenye misimamo mikali. Katika miaka ya hivi karibuni, wakuu wa sasa na wa zamani wa Afghanistan wamekuwa wakisema kuwa helikopta za kigeni zinaingiza kwa siri silaha na magaidi nchini humo.

Ukweli wa mambo ni kuwa,  hivi sasa wakati Afghanistan ikianza kuingia katika muongo wa tatu tokea ikaliwe kwa mabavu na askari wa kigeni wanaoongozwa na Marekani inakabiliwa na mustakbali mgumu. Inasikitisha sana kuwa wananchi wa Afghanistan ni waathirika wakuu wa ushirikiano wa Marekani na magaidi. Ushirikiano huo umebainika wazi baada ya Trump kukiri kuwa uwepo wa majeshi ya nchi yake Afghanistan ni kwa faida ya Taliban na wala si kwa ajili ya maslahi ya watu wa  Afghanistan .

 

Tags

Maoni