May 22, 2020 06:30 UTC
  • Russia na Venezuela zakosoa hatua zisizo za kisheria za Marekani

Tangu Rais Donald Trump mwenye kashfa nyingi wa Marekani aingie ikulu ya White House ameshadidisha siasa za uhasama dhidi ya Venezuela ambapo pia amefanya njama nyingi za kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Nicolás Maduro wa nchi hiyo sambamba na kuiwekea vikwazo vikali.

Vikwazo hivyo vimeifanya serikali ya Caracas kuomba msaada kutoka kwa marafiki zake ikiwemo Iran lakini pamoja na hayo Washington imeendeleza ukwamishaji mambo wake na sasa inajaribu kuzuia kufika msaada huo kwa nchi hiyo. Suala hilo limepelekea kutolewa radiamali hasi kutoka kwa Venezuela na Russia. Katika uwanja huo, wawakilishi wa Venezuela na Russia katika Umoja wa Mataifa wametoa radiamali kali kuhusiana na vitisho vya Marekani dhidi ya meli za mafuta za Iran. Mwakilishi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa sambamba na kuashiria vitisho vya Marekani vya kutumia nguvu dhidi ya meli tano za mafuta za Iran zilizo njiani kuelekea Venezuela amesisitiza kwamba, vitisho hivyo vya kutumia nguvu dhidi ya meli za Iran vinakiuka sheria za kimataifa, uhuru wa biashara na safari za baharini. Naye mwakilishi wa Russia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amesema, anatumai kwamba Washington itafahamu hatari ya kuweka meli za kivita za Marekani katika eneo ambalo kuna meli za mafuta za Iran. Kabla ya matamshi hayo, Waziri wa Ulinzi wa Venezuela alikuwa ameashiria kwamba meli za kivita za nchi yake zitazishindikiza meli hizo za Iran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika kuiunga mkono Venezuela imetuma meli tano zilizosheheni mafuta kupitia lango bahari la Jabal Tariq (Gibraltar) na maji ya kimataifa kuelekea nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Viongozi wa Marekani wanadai kwamba mauzo ya mafuta ya Iran kwa Venezuela ni kinyume cha sheria na kwamba ni lazima wakabiliane na suala hilo. Ni kwa msingi huo ndipo wakatuma askari wa baharini wa Marekani karibu na maji ya Venezuela.

Msafara wa meli za mafuta

Hatua hiyo ya Marekani imekabiliwa na radiamali kali ya Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela ambaye ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter akilalamikia kitendo hicho cha Washington kufuatilia meli za mafuta za Iran zinazoelekea nchini kwake. Amesema, katika kipindi hiki cha kuenea virusi vya Corona Washington inafuatilia meli zinazotuletea mafuta. Huu ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na haki ya msingi ya watu wa Venezuela. Ukweli ni kwamba hatua hiyo ya Washington yaani ya kujaribu kuzuia meli za Iran zilizobeba mafuta kuelekea Venezuela kwa kisingizio cha vikwazo vya upande mmoja vya serikali ya Rais Donald Trump dhidi ya nchi nyingine, ni hatua iliyo kinyume cha sheria kikamilifu na kinyume na misingi ya kimataifa. Hii ni kusema kuwa vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Venezuela na Iran, vinapasa kufanya kazi ndani ya mipaka ya Marekani tu na si kinyume chake. Hii ni katika hali ambayo serikali ya Trump hivi sasa inajaribu kusumbua na kuzizuia meli za Iran zilizoko katika maji ya kimataifa kuweza kutia nanga katika bandari za Venezuela. Kwa mtazamo wa sheria za kimataifa, uwepo wa meli za kivita za Marekani karibu na maji ya Venezuela na kujaribu kukabiliana na meli za mafuta za Iran, ni tishio kwa safari za meli na ambalo linakiuka wazi sheria za baharini za mwaka 1982. Ni wazi kwamba hatua hiyo inaweza kusababisha mzozo mkubwa katika eneo la Caribbean. Kitendo hicho cha serikali ya Trump kinajiri katika fremu ya ubabe wa Washington wa kutumia mabavu katika uga wa kimataifa kwa ajili ya kifikia malengo yake machafu. Katika uwanja huo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tayari imekwishatoa tamko kali na kuonya juu ya uchokozi na chokochoko zozote za serikali ya Trump kuhusiana na suala hilo.

Juhudi zilizogonga mwamba za Trump kujaribu kuzuia uuzwaji mafuta ya Iran

Katika uwanja huo Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sambamba na kumuandikia barua António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya vikali uingiliaji kijeshi wa Marekani katika suala la uagizaji mafuta kutoka Iran kwenda Venezuela na kusema kuwa hatua ya Washington ya kutoa vitisho visivyo vya kisheria na kuzifuatilia meli za mafuta za Iran ni aina fulani ya uharamia wa baharini unaohatarisha amani na usalama wa kimataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Marekani inapaswa kuhitimisha vitisho vyake vya kimataifa na badala yake iheshimu sheria za uhuru wa safari za meli katika maji ya kimataifa." Msimamo mkali wa Iran kuhusiana na hatua yoyote ya Marekani iliyo kinyume cha sheria imeifanya Washington kulegeza msimamo wake wa awali wa kukabiliana moja kwa moja na meli za Iran na badala yake kutumia vitisho laini. Katika uwanja huo Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na katika kikao na waandishi wa habari sambamba na kukariri madai na tuhuma bandia dhidi ya Iran ameionya jamii ya kimataifa dhidi ya kufanya biashara za meli na Iran na kudai kwamba biashara hizo zitakuwa na matokeo mabaya sana. Licha ya vitisho hivyo vya Washington, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kupanua uhusiano na waitifaki wake ikiwemo Venezuela sambamba na kupuuzilia mbali bwabwaja za watawala wa Washington.

Tags

Maoni