May 22, 2020 07:57 UTC
  • UN yakanusha madai ya US kwamba inatumia corona kuhamasisha uaviaji mimba

Umoja wa Mataifa umekanusha vikali madai ya Marekani kuwa taasisi hiyo ya kimataifa inatumia janga la corona kuhamasisha uaviaji mimba duniani.

Msemaji wa UN, Stephane Dujarric jana Alkhamisi katika kikao na waandishi wa habari mjini New York alisema, "wazo lolote kwamba tunatumia janga la Covid-19 kuhamasisha utoaji wa mimba halina ukweli wowote."

Amesema, katika hali ambayo Umoja wa Mataifa unaunga mkono mfumo wa afya unaozuia mamilioni wa wanawake kupoteza maisha wakati wa ujauzito na pia wakati wa kujifungua, sambamba na kuzuia watu wasipate magonjwa ya zinaa, lakini hauna azma ya kukanyaga sheria zozote za kitaifa.

Katika barua yake siku ya Jumatatu kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, John Barsa, Mratibu wa shirika la misaada la Marekani la USAID alidai kuwa, UN haipaswi kutumia janga la corona kushajiisha uaviaji wa mimba na kuutaja kama hudumu nyeti.

Marekani ndiye muathirika mkubwa zaidi wa janga la corona duniani

Hata hivyo Umoja wa Mataifa umepuuzilia madai hayo ya Marekani na kusema kuwa, inahitaji dola bilioni 6.7 kwa ajili ya kuzisaidia nchi 63 hususan za Afrika na Amerika ya Latini, ili kuzuia ueneaji wa virusi vya corona na athari hatarishi za janga la corona.

Zaidi ya watu milioni tano wamekumbwa na virusi vya corona kote duniani kufikia sasa, mbali na wengine zaidi ya 327,000 kuaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19.

 

Tags

Maoni