May 22, 2020 09:48 UTC
  • Siku ya Quds na kuongezeka makabiliano ya Wapalestina na  'Muamala wa Karne'

Katika Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu 2020, Wapalestina wameimarisha harakati zao za kupinga mpango wa kibaguzi unaojulikana kama 'Muamala wa Karne'.

Imepita miaka 72 tokea uasisiwe utawala bandia wa Israel katika ardhi za Wapalestina. Utawala wa Kizayuni wa Israel umetekeleza kila aina ya jinai dhidi ya Wapalestina katika miaka hiyo 72. Hakuna chochote kilichonusurika na jinai za Israel kwani utawala huo bandia umelenga jiografia, historia na dini ya watu wa Palestina.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kuwalazimisha Wapalestina kuondoka katika ardhi zao hizo za jadi. Aidha utawala wa Kizayuni unapotosha historia ya Palestina kwa lengo la kuvuruga utambulisho wa kidini wa Wapalestina na kuzipa sura bandia ya Uyahudi ardhi  na maeneo matukufu ya Palestina na njama hizo hasa zimelenga mji mtakatifu wa Quds (Jerusalem).

Wakaazi milioni sita wa Palestina wamelazimika kuwa wakimbizi baada ya Israel kuteka na kupora ardhi zao. Hivi sasa Wapalestina wanaishi katika kambi za wakimbizi na makumi ya maelefu ya wengine wameuawa shahidi huku malaki ya wengine wakijeruhiwa katika hujuma za Israel. Miongoni mwa Wapalestina waliouawa shahidi au kujeruhiwa katika hujuma za utawala wa Kizayuni  wa Israel ni wanawake na watoto wadogo. Kwa mfano katika miongo miwili ya kwanza ya karne ya 21 utawala katili wa Israel umewaua shahidi watoto elfu 3 Wapalestina na kuwajeruhi wengine 13,000 huku watoto wengine 12,000 wakikamatwa na kufungwa katika jela za kuogofya za Israel.

Pamoja na kuwepo jinai zote hizo, baadhi ya makundi ya Palestina hasa Mamlaka ya Ndani ya Palestina yamekuwa na imani potovu kuwa kuna uwezekano wa kupunguza jinai hizo za utawala wa Kizayuni kwa njia ya mazungumzo na maelewano na utawala huo.

Msikiti wa Al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala bandia wa Israel

Mpango wa kibaguzi wa ‘Muamala wa Karne’ ambao ulizinduliwa na rais Donald Trump wa Marekani umethibitisha wazi kuwa gharama ya kuwa na uhusiano na utawala wa Israel ni ghali zaidi kuliko mapambano na muqawama. Kimsingi ni kuwa, ‘Muamala wa Karne’ ni gharama iliyotwishwa Palestina na wale wenye msimamo wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo wa Kizayuni wa Israel. Mapatano ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel na mwanasiasa anayeshirikiana naye katika utawala, Benny Gantz, kuhusu kuunganishwa sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, yaani Israel, kuanzia Juni Mosi ni jambo ambalo limethibitisha kuwa, muelekeo wa kukalia mabavu ardhi za Palestina hauhusu tu shakhsia maalumu wa Kizayuni bali mawaziri wakuu wote wa Israel wanafuatilia lengo la kujitanua na kupora ardhi zaidi za Wapalestina.

Inaelekea kuwa, Wapalestina ambao walikuwa wanafuatilia sera ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wamefikia natija kuwa, mchakato wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala huo bandia umefika ukingoni.

Ni kwa msingi huu ndio Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Jumamosi iliyopita, katika radiamali yake kuhusu uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kupora maeneo zaidi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuyaunganisha na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, akaatangaza bayana kuwa, Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) na Mamlaka ya Ndani ya Palestina hazitafungamana tena na mapatano yake na Marekani na Israel.

Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina

Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mohammad Shtayyeh siku ya Jumatano katika kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri alitoa amri ya kuchukuliwa hatua za haraka kutekeleza kivitendo uamuzi wa Mahmoud Abbas wa kukata uhusiano na utawala wa Kizayuni pamoja na Palestina kufuta mapatano yote ya amani.

Mbali na hayo, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imefikia natija kuwa, jitihada za baadhi ya nchi za Kiarabu za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni jambo ambalo limeupa utawala huo kiburi cha kuteka ardhi zaidi za Ukingo wa Magharibi. Kwa msingi huo, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekataa kupokea misaada ya kitiba ya Umoja wa Falme za Kiarabu kwa sababu misaada hiyo ilikuwa iwafikieWapalestina kupitia uwanja wa ndege wa Tel Aviv, mji mkuu wa utawala bandia wa Israel.

Hatua hii ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo ilichukuliwa wakati wa kukaribia Siku ya Kimataifa ya Quds imesadifiana na sisitizo la harakati za muqawama na mapambano ya Kiislamu za Palestina kuhusu kufungamana na malengo matakatifu ya ukombozi wa Quds.

Kwa maelezo hayo, tunaweza kusema kuwa, ingawa hakukuwa na mijumuiko mikubwa katika miji mbali mbali katika Siku ya Kimataifa ya Quds kutokana na janga la corona, lakini kumeshuhudiwa kuimarika msimamo na kauli moja miongoni mwa Wapalestina kuhusu udharura wa kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel na ‘Muamala wa Karne’.

 

Tags

Maoni