May 23, 2020 07:15 UTC
  • Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran; jitihada zisizo na tija za utawala wa Trump

Baada ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran mnamo Mei 2018, serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani imekuwa ikitekeleza mashinikizo ya juu kabisa kwa kuiwekea Iran vikwazo shadidi zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia. Pamoja na kuwa vikwazo hivyo havijaweza kufanikiwa, Marekani inasisitiza kuendelea na sera yake hiyo ya vikwazo.

Katika hatua ya hivi karibuni kabisa ya vikwazo vyake, serikali ya Trump imewawekea vikwazo maafisa wa Iran na taasisi kadhaaa za nchi hii.

Idara ya Udhibiti wa Mali katika Wizara ya Fedha ya Marekani Jumatano ilitangaza vikwazo vipya dhidi ya Iran. Katika orodha iliyowekwa katika tovuti ya Wizara ya Fedha ya Marekani, kuna majina ya watu 9 Wairani na taasisi tatu za Iran. Mara hii vikwazo vya Marekani vimemlenga Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran na Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi hilo wakiwemo makamanda na baadhi ya manaibu wao pamoja na magereza mawili.

Washington imedai kuwa eti kwa kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi katika historia, ambavyo  vinawekwa katika fremu ya mashinikizo ya juu kabisa, itailazimisha Iran kusalimu amri na hivyo kutii matakwa 12 ambayo yalitangazwa na Pompeo Mei 2018. Pamoja na hayo, taifa la Iran limeonyesha mapambano na muqawama wa aina yake mbele ya vikwazo hivyo. Ni kwa msingi huo ndio Marekani sasa imebakia kuchukua hatua za kichochezi kama vile kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika orodha yake ya makundi ya ‘kigaidi’, kumuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC na kuwawekea vikwazo maafisa wa ngazi za juu wa Iran. Aidha mara kwa mara Marekani huwawekea vikwazo watu mbali mbali kwa kisingizio cha kuisaidia Iran katika uuzaji bidhaa ambazo zimewekewa vikwazo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Abdolreza Rahmani Fazli

Katika vikwazo vipya, Marekani imewawekea vikwazo maafisa wanaohusika na masuala ya polisi na usalama wa ndani nchini Iran. Katika kutathmini hatua hiyo ya Marekani tunaweza kusema kuwa,  katika fremu yake ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran, Marekani imewawekea vikwazo maafisa mbali mbali wa Iran pamoja na taasisi muhimu za nchi hii. Vikwazo hivyo vimeenea katika sekta zote na sasa Marekani haina machaguo mengine ya vikwazo na ndio sababu baada ya kumuwekea vikwazo waziri wa mambo ya ndani, makamanda na manaibu makamanda wa Jeshi la Polisi la Iran mara hii wameweka vikwazo dhidi ya magereza mawili na nukta hiyo inaonyesha kufilisika kimawazo wakuu wa Washington.

Swali ambalo linaibuka hapa ni hili kwamba je, msingi wa vikwazo hivi una uhusiano gani katika kuongeza taathira ya hatua hasimu za utawala wa Trump dhidi ya Iran?

Hata baada ya kuibuka janga la COVID-19 au corona, si tu kuwa Marekani haijaondoa vikwazo vyake vya kidhalimu dhidi ya Iran bali imeongeza zaidi vikwazo hivyo kwa lengo la kuidhuru Iran ili kwa dhana yake potovu, iilazimishe Tehran isalimu amri na kutii matakwa yake haramu. Wakuu wa Washington wanadhani kuwa mashinikizo yao ya juu kabisa dhidi ya Iran yamezaa matunda. Brian Hook, mkuu wa masuala ya Iran katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mnamo 19 Mei alisema Iran ina njia moja tu mkabala wa Marekani. Aliongeza kuwa ni miaka mitatu sasa ambapo Marekani imekuwa ikikabiliana na Iran kwa njia za vikwazo na mashinikizo. Aidha amedai kuwa kutokana na vikwazo hivyo sasa Iran imepata pigo na kushindwa. Ameendelea kusema viongozi wa Iran wana chaguo moja tu, ima wafanye mazungumzo na Rais Trump au wadhibiti uporomokaji wa uchumi wa nchi yao.

Brian Hook, mkuu wa masuala ya Iran katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani  (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa utawala bandia wa Israel Benjamin Netanyahu

Haya madai ya Brian Hook hayajazingatia uhalisia wa mambo kwani Iran imeweza kusimama kidete mbele ya mashinikizo ya pande zote ya Marekani kwa kutekeleza sera za uchumi wa kimapambano au kimuqawama.

Seneta wa chama cha upinzani cha Democrat Chris Murphy anaamini kuwa: “Trump alivuruga mapatano ya nyuklia (ya JCPOA) na kuahidi kuwa angeleta mfumo mpya wa kimataifa wa mashinikizo ili kuilazimisha Iran iafiki mapatano mapya. Mpango huo umefeli kwa madhila na hakuna yeyote aliyejiunga na vikwazo vipya vya Trump dhidi ya Iran. Hivi sasa Iran inaendelea na mpango wake wa nyuklia na hakuna mapatano mapya yaliyoweza kufikiwa.

Kwa hakika, pamoja na kelele nyingi ambazo utawala wa Trump umeziibua, ukweli ni kuwa haujafanikiwa katika sera zake kuhusu Iran na licha ya matamshi ya kipropaganda ya Trump na wakuu wa utawala wake, imebainika kuwa sera za mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran zimegonga mwamba.

Tags

Maoni