May 23, 2020 07:59 UTC
  • Corona yawakatizia watoto milioni 80 chanjo za polio, surua na kipindupindu

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa janga la corona limevuruga mpango wa utoaji wa chanjo za magonjwa ya kupooza (polio), surua na kipindupindu kwa makumi ya mamilioni ya watoto duniani.

Katika ripoti yake mpya ya jana Ijumaa, WHO imesema watoto karibu milioni 80 wenye chini ya umri wa mwaka mmoja wapo katika hatari ya kupoteza maisha iwapo watakosa chanjo hizo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema katika taarifa kuwa, "kukatizwa utoaji wa chanjo kutokana na janga la Covid-19 kunahatarisha kusambaratisha mafanikio yaliyopatikana ndani ya miongo kadhaa iliyopita, katika kukabiliana na magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo kama vile surua."

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema kusimamishwa safari za ndege na kuwekwa sheria kali za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 (Corona) kumepelekea kusimama kwa sughuli za ufikishaji na utoaji wa chanjo katika nchi zinazohitaji hususan za Kiafrika.

Dozi moja ya chanjo ya surua (measles)

Inaarifiwa kuwa, kampeni 46 za utoaji wa chanjo ya kupooza kwa watoto zimesimamishwa katika nchi 38 duniani hususan za Afrika, baada ya nchi hizo kusimamisha safari zake za ndege ili kuzuia ueneaji wa corona.

Shirika la Afya Duniani (WHO) Mei mwaka jana lilitangaza huko nyuma kuwa, huenda likatangaza karibuni hivi kuwa bara Afrika halina tena ugonjwa wa kupooza wa Polio. Awali bara hilo lilikuwa limeanzia kuutokomeza ugonjwa huo kufikia mwaka 2000.

 

Tags

Maoni