May 23, 2020 09:17 UTC
  • Russia: Tutafanya juhudi zote kuzuia kuongezewa muda vikwazo vya silaha vya Iran

Russia imesisitiza kuwa, itafanya juhudi zake zote kuhakikisha kuwa Umoja wa Mataifa haurefushi vikwazo vyake vya silaha dhidi ya Iran baada ya tarehe 18 Oktoba 2020, bali unatekeleza kivitendo azimio lake la kuindolea Tehran vikwazo hivyo kwa mujibu wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Sergey Ribakov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Rusia amesema hayo na kuongeza kuwa, kusema kweli hali iliyopo hivi sasa kuhusu marufuku ya kuiuzia silaha Iran ni muendelezo wa vikwazo vya silaha dhidi ya Tehran ambavyo kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inabidi viondolewe ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka huu.

 

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia aidha amesema: Sidhani kwamba baada ya tarehe 18 Oktoba 2020 bado utakuwepo mfumo wa vikwazo kwa sura yoyote ile wa kuweza kuzuia mauzo ya silaha kwa Iran, kwa mujibu wa vielelezo saba vya masuala ya silaha vinavyotambuliwa na Umoja wa Mataifa. Pia amesema uhusiano wa nchi yake na Marekani si tete tu, bali umekumbwa na mvurugiko mkubwa na jambo hilo linatokana na matatizo ya ndani ya Marekani wakati huu wa kukaribia hivi sasa kufanyika uchaguzi mwingine wa rais unaotarajiwa kufanyika tarehe tatu Novemba mwaka huu. 

Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasema kuwa, muda wa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran unamalizika taerhe 18 Oktoba mwaka huu wa 2020 kulingana na mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Hata hivyo Marekani inafanya njama kubwa za kuhakikisha vikwazo hivyo haviondolewi, na inafanya juu chini kuhakikisha kuwa muda huo unarefushwa.

Maoni