May 24, 2020 02:44 UTC
  • Venezuela yaionya tena Marekani kuhusu vitisho dhidi ya meli za mafuta za Iran

Mwakilishi wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa sambamba na kuionya Marekani, amesisitiza kuwa vitisho vya kijeshi vinavyotolewa na Washington dhidi ya meli za mafuta za Iran, havikubaliki.

Samuel Moncada aliyasema hayo Jumamosi na kuongeza kwamba, Marekani imetishia kutumia nguvu ya kijeshi dhidi ya meli za mafuta za Iran zilizo njiani kuelekea Venezuela. Moncada ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, shambulizi lolote dhidi ya meli za mafuta ambazo zinatumia haki ya biashara huria na uhalali wa safari za meli kati ya nchi huru, linahesabika kuwa uchokozi na jinai. Katika uwanja huo jeshi la Venezuela katika kuionyesha Marekani uwezo wake wa kijeshi limefanya maneva ya makombora katika kisiwa ambacho meli za mafuta za Iran zinasubiriwa. Ijumaa Rais Nicolás Maduro wa Venezuela alithibisha kuwa jeshi la nchi hiyo limefanya maneva katika kisiwa hicho cha Orchila.

Samuel Moncada, Mwakulishi wa Venezuela Katika Umoja wa Mataifa

Kuimarika uhusiano wa Tehran na Caracas, pande mbili muhimu ambazo zimekuwa zikiandamwa na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani, kumewatia hofu na wahka mkubwa viongozi wa White House ambapo baada ya kuanza safari za meli za Iran zilizobeba mafuta kuelekea Venezuela Washington ilituma askari wake katika bahari ya Caribbean kwa lengo la kuzisumbua au kuzizuia meli hizo zisike katika nchi hiyo. Kufuatia hatua hiyo Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alimwandikia barua António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akionya vikali kuhusu vitisho hivyo vilivyo kinyume cha sheria na hatari vya Marekani na kusema ni aina fulani ya uharamia wa baharini unaohatarisha amani na usalama wa kimataifa.

Tags

Maoni