May 24, 2020 08:55 UTC
  • Maneva ya mizinga ya jeshi la Venezuela katika kukaribia kuwasili meli za mafuta za Iran katika maji ya Caribbean

Katika hali ambayo ikulu ya Marekani ya White House inatekeleza vikwazo vikali zaidi vilivyo kinyume na ubinaadamu dhidi ya raia na serikali ya Venezuela kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Nicolás Maduro, kuongezeka ushirikiano wa kibiashara kati ya Tehran na Caracas na kutumwa meli za mafuta zilizosheheni nishati hiyo muhimu huko Venezuela, kumewaongezea hasira viongozi wa Marekani.

Kiasi cha kuwafanya baadhi ya viongozi wa Marekani watoe vitisho dhidi ya Venezuela na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vitisho vya viongozi wa Marekani vimelilazimu jeshi la Venezuela kufanya maneva katika kisiwa cha Orchila kwa lengo la kuionyesha Marekani uwezo wake wa kijeshi huku likisubiri kuzisindikiza meli za mafuta za Iran. Katika uwanja huo Rais Nicolás Maduro wa Venezuela amesema kuwa, jeshi hilo limeyafanyia majaribio makombora yake ya kulenga shabaha katika maneva yake kwenye kisiwa hicho. Maneva hiyo imefanyika katika fremu ya mpango uliopewa jina la 'Ngao ya Bolivia' ambapo jeshi la Venezuela litaendelea kupiga kambi katika kisiwa cha Orchila. Kuimarika uhusiano wa Tehran na Caracas, pande mbili muhimu ambazo zimekuwa zikiandamwa na vikwazo vya kidhalimu vya Marekani, kumewatia hofu na wahka mkubwa viongozi wa White House. Kuhusiana na suala hilo Robert O'Brien, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ambapo sambamba na kukariri madai yake yasiyo na msingi dhidi ya serikali ya Rais Nicolás Maduro amesema: "Kuagiza mafuta ya Iran ni hatua ya kukataa tamaa ambayo imechukulia na utawala fasidi na usio wa kisheria wa Maduro." 

Maneva ya mizinga ya jeshi la Venezuela

Inafaa kuashiria kwamba baada ya kuanza safari meli za Iran zilizobeba mafuta kuelekea Venezuela Washington ilituma askari wake wa mahini katika bahari ya Caribbean kwa lengo la kuzisumbua au kuzizuia meli hizo zisifike katika nchi hiyo, huku baadhi ya viongozi wa Marekani wakitoa vitisho kwamba, walikuwa wanachunguza hatua zinazofaa ambazo wangezichukua kwa lengo la kutoa radiamali kufuatia kuagizwa mafuta ya Iran kwenda nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Marekani inatumia vitisho dhidi ya nchi mbili za Iran na Venezuela katika hali ambayo, siasa hizo zinakiuka wazi misingi na sheria za kimataifa za biashara huria na sheria za safari za meli. Kama alivyoashiria Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika barua aliyomwandikia António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, vitisho hivyo vilivyo kinyume cha sheria, hatari na uchokozi wa Marekani ni aina fulani ya uharamia wa baharini unaohatarisha amani na usalama wa kimataifa. Hivi sasa jeshi la Venezuela limefanya maneva ya kuonyesha uwezo wake wa kijeshi huku Vladimir Padrino López, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo akitangaza kwamba baada ya meli za Iran zilizobeba mafuta kuingia katika maji ya Venezuela zitasindikizwa na meli za kivita za nchi hiyo. Hata kama kwa muda sasa Venezuela imekuwa chini ya mashinikizo makali ya Marekani, lakini imeweza kutatua baadhi ya migogoro na matatizo ya kiuchumi kwa kumarisha miamala ya kimataifa na nchi zisizo washirika na Marekani.

Utayarifu wa viongozi na jeshi la Venezuela umewatia hofu watawala wa Marekani

Katika uwanja huo, kupanua uhusiano na China, Russia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kumeisaidia sana serikali ya Caracas kuweza kutatua baadhi ya matatizo makubwa yanayoikabili, suala ambalo ni kinyume na matarajio ya viongozi wa Marekani. Kwa miaka kadhaa sasa viongozi wa Marekani si tu kwamba wametekeleza siasa chafu tofauti zikiwemo za kufunga njia muhimu za kufikisha misaada nchini Venezuela, bali hata wamewaunga mkono wapinzani wa ndani sambamba na kutekeleza uharibifu mkubwa kwenye mitambo ya kuzalisha umeme na taasisi muhimu za kimaisha zinazowahudumia raia wa nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, Jorge Arreaza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela sambamba na kuashiria hatua za uadui za Marekani katika miaka ya hivi karibuni dhidi ya serikali ya Caracas, amesisitiza kwamba White House imeendesha vita tofauti dhidi ya Venezuela ili iweze kudhibiti vyanzo vya maliasili na siasa za nchi hiyo. Hata kama njama za Marekani za kuiondoa madarakani serikali ya mrengo wa kushoto ya Rais Nicolás Maduro bado zinaendelea, lakini vitisho vya Washington bado havijawa na natija yoyote. Aidha katika kadhia ya hivi sasa, hatua ya jeshi la Venezuela ya kufanya maneva ya kijeshi na kutangaza azma yake ya kuzisindikiza meli za mafuta za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa mara nyingine imeonyesha msimamo imara wa nchi hiyo mkabala wa vitisho hivyo vya Marekani. Hii ni katika hali ambayo meli ya kwanza ya Iran iliyobeba mafuta imefanikiwa kutia nanga nchini Venezuela, huku zingine zikiendelea na safari zao kuelekea nchi hiyo.

Tags

Maoni