May 25, 2020 06:50 UTC
  • China yapinga kulipa hasara kwa sababu ya kuenea virusi vya Corona

Waziri wa Mambo ya Nje wa China amejibu matamshi ya viongozi wa Marekani kwamba serikali ya Beijing inatakiwa kulipa hasara inayotokana na kuenea virusi vya Corona na kusisitiza kuwa, kupata fidia kutoka China ni 'njozi batili.'

Wang Yi ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari kilichofanyika Jumapili kando ya mkutano wa kila mwaka wa chama cha Kongresi ya Watu wa China, kilichofanyika kwa njia ya video mjini Beijing ambapo amesema kuwa virusi vya Corona havina mpaka wala taifa. Aidha amevitaja virusi hivyo kuwa changamoto ya pamoja ya kibinaadamu na kwamba kitendo cha kuingizwa siasa, kujitenga na kutozingatia masuala ya elimu, kutashadidisha zaidi ugonjwa huo.

Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China

Waziri wa Mambo ya Nje wa China ameongeza kwamba Rais Xi Jinping wa nchi hiyo mara nyingi amevitaja virusi hivyo kuwa ni adui wa pamoja wa mwanaamu ambaye atashindwa kwa kuwepo mshikamano na ushirikiano. Katika wiki za hivi karibuni serikali ya Marekani imekuwa ikikariri ukosoaji wake kuhusu usimamizi mbaya katika kuenea virusi vya Corona mjini Wuhan nchini China na kudai kwamba kuenea virusi hivyo kunatokana na udhaifu wa usimamizi wa nchi hiyo na hivyo kuitaka ifidie hasara iliyozipata nchi zilizoathirika na maradhi hayo.

Tags

Maoni