May 27, 2020 15:51 UTC
  • Russia yakanusha madai ya US ya kutuma ndege za kivita Libya

Russia imekadhibisha na kutaja kama upotoshaji madai ya Marekani kwamba Mosow imetuma ndege za kijeshi nchini Libya kwenda kuwasaidia wapiganaji wa Khalifa Haftar.

Andrey Krasov, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge la Russia (Duma) amesema tuhuma hizo za Marekani haziakisi ukweli wa mambo.

Amesema "msimamo wa Russia unajulikana wazi; sisi tunaunga mkono kumalizika umwagwaji damu Libya, tunaziomba pande zote husika katika mgogoro wa Libya kujiepusha na utumiaji wa silaha na kuketi katika meza ya mazungumzo."

Kauli hiyo ya Moscow ni radimali kwa madai yaliyotolewa Jumanne ya jana na Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) kwamba ndege za kijeshi za Russia zimewasili Libya zikitokea uwanja wa ndege wa kijeshi wa Russia kupitia Syria.

Wanamgambo wa Khalifa Haftar

Kamanda mkuu wa AFRICOM Jenerali Stephen Townsend alidai kuwa ndege hizo za kivita za Russia yumkini zimeenda Libya ili kutoa usaidizi na ufuatiliaji wa karibu wa mashambulizi ya anga kwa 'mamluki' wa Russia ambao eti wanashirikiana na wapiganaji wa kundi linalojiita 'Jeshi la Taifa ya Libya' linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar.

Kundi hilo linalojiita Jeshi la Kitaifa la Libya ambalo kwa miaka kadhaa sasa limekuwa likiungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi huku likiendesha shughuli zake mashariki mwa Libya, lilianzisha mashambulizi makali dhidi ya mji wa Tripoli kuanzia mwezi Aprili mwaka jana, kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji huo.

Tags

Maoni