May 31, 2020 02:24 UTC
  • Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani, sababu na hatari zake

Marekani imetumbukia tena katika machafuko makubwa kutokana na malalamiko ya wananchi wanaopinga mauaji yaliyofanywa na polisi wa nchi hiyo dhidi ya raia mweusi.

Katika kipindi cha siku nne zilizopita miji mbalimbali ya Marekani kuanzia Minneapolis hadi New York, Atlanta mpaka Houston na Milwaukee hadi Los Angeles imekumbwa na maandamano na ghasia kubwa baina ya raia wanaoandamana, na polisi. Watu kadhaa wamejeruhiwa katika baadhi ya machafuko hayo na kunashuhudiwa ghasia na hata oporaji wa maduka katika miji mingine. 

Inatupasa kusema hapa kuwa, kinachoshuhudiwa sasa nchini Marekani si hasira na vuguvugu la kupita tu la kulalamikia mauaji yaliyofanywa na polisi dhidi ya raia mweusi, George Floyd, aliyegandamizwa na kubinywa shingo na afisa wa polisi hadi kufa katika mji wa Minneapolis, bali ni mlipuko wa hasira za mamia ya miaka ya ukandamiza, dhulma na ubaguzi uliokita mizizi katika jamii ya Marekani dhidi ya watu weusi na jamii za waliowachache.

  Meya wa New York, Andrew Cuomo anasema: "Yanayojiri sasa huko Minneapolis si matukio ya ghafla ya kupita tu, bali ni ukurasa mwingine wa kitabu cha dhulma na ubaguzi wa kudumu nchini Marekani." 

Image Caption

Kitabu hiki kilianza kuandikwa miaka ya kabla ya kuasisiwa Marekani kwa mauaji ya Wahindi Wekundu na kuanza kwa biashara ya utumwa katika makoloni ya Uingereza katika ulimwengu mpya na kilinaendelea kuandikwa kwa kipindi cha miaka 400 kwa aina mbalimbali za dhulma, unyanyasaji na ukatili dhidi ya jamii za watu asili au jamii za waliowachache. Raia wa Marekani wamekuwa wakimiminika mitaani kupinga dhulma na ukatili huo mara kwa mara ili asaa wakafanikiwa kubadili au kuondoa kabisa hali hiyo; lakini inasikitisha kuwa mara zote mapambano hayo ya kupigania haki za kijamii yamekuwa yakizimwa na kukandamizwa na vikosi vya usalama au kuvurugwa na baadhi ya makundi ya waporaji na wahuni.

Kwa bahati nzuri katika miaka ya hivi karibuni na kutokana na kustawi kwa vyombo vya habari na harakati za mitandao ya kijamii, kumekuwepo uwezekano wa kushuhudia habari za ndani zaidi na kiwango cha dhulma na ukatili mkubwa unaofanywa na vyombo vya dola vya Marekani dhidi ya raia weusi wa nchi hiyo na vilevile kuakisi umoja na mshikamano uliopo baina ya wapinzani wa ukatili na ubaguzi huo. Ni katika mazingira haya ndipo kukaibuka harakani maarufu ya "Black Lives Matter" inayowatetea Wamarekani weusi ambayo pia inawashirikisha Wamarekani wazungu. Harakati hii inafanya jitihada za kuhakikisha kwamba, Wamarekani weusi wanapata mafanikio ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kushirikishwa au kupewa vyeo na nafasi muhimu nchini Marekani kama cheo cha rais wa nchi, na kufuta ubaguzi na umaskini mkubwa unaoshuhudiwa katika jamii zao. Lengo hili linapata umuhimu zaidi kwa kutambua kuwa, miaka mingi ya utumwa na siasa za ubaguzi wa kimbari imeeneza na kuimarisha zaidi utamaduni wa dhulma, ubaguzi na ukatili katika jamii ya nchi hiyo. Na hapana shaka kuwa ni muhali kuweza kusitisha mauaji na ukatili unaofanywa na polisi wazungu wanaokingiwa kifua na vyombo vya dola dhidi ya Wamarekani weusi bila kwanza kubadilisha utamaduni wa fikra za kibaguzi baina ya Wamarekani.

Image Caption

Sambamba na harakati kubwa ya kudai haki za kijamii na kiraia za Warekani weusi na jamii za wachache na kupinga ubaguzi nchini Marekani, kunashuhudiwa harakati la makundi ya wabaguzi ambazo zimeshika kasi zaidi katika kipindi cha utawala wa sasa kwa shabaha ya kulinda "turathi" habithi ya ubaguzi wa rangi nchini humo. Wafuasi wa kundi hilo hawasiti hata kuwakanyaga kwa magari au kuwapiga risasi vinara wa harakani ya kupinga ubaguzi. Harakati za makundi haya ya kibaguzi zimeshadidi zaidi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita kutokana na matamshi ya kichochezi ya Rais Donald Trump wa Marekani kwa kadiri kwamba, hata wasimamizi wa mtandao wa kijamii wa Twitter wamezitaja jumbe za Trump katika mtandao huo kuwa zinakiuka sheria kwa kusifia na kuchochea ukatili na wamezuia kutumwa tena au kubonyeza kitufe kinachoonesha kuunga mkono jumbe hizo.

Image Caption

Alaa kulli hal, kuendelea kwa mgogoro mkubwa wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani kumeitumbukiza tena nchi hiyo katika machafuko makubwa ya kisiasa na kijamii, na kwa kutilia maanani hali mbaya ya kiuchumi iliyozidishwa na mlipuko wa virusi vya corona, hapana shaka kuwa, suala hili litasababisha hatari kubwa zaidi na kuzusha mtikisiko mkubwa katika muundo wa jamii ya nchi hiyo.

Tags

Maoni