May 31, 2020 11:46 UTC
  • Maandamano, ghasia zashtadi Marekani licha ya 'kafyu' na kamatakamata

Licha ya agizo la kutotoka nje usiku na kukamatwa mamia ya waandamanaji, lakini maandamano ya kulaani ubaguzi wa rangi na jinai ya polisi mweupe kumuuua Mmarekani mwenye asili ya Afrika, yameendelea kushuhudiwa katika miji na majimbo mbalimbali ya Marekani.

Miji mbalimbali ya Marekani imekumbwa na wimbi la maandamano na machafuko makubwa yaliyochochewa na mauaji yaliyofanywa na polisi katika mji wa Minneapolis jimbo la Minnessota dhidi ya raia mwenye asili ya Afrika, George Floyd. 

Usiku wa kuamkia leo, Gavana Gavin Newsom wa jimbo la California alitangaza 'hali ya hatari' katika kaunti ya Los Angeles kufuatia kushtadi ghasia na machafuko ya kulalamikia ukatili huo wa polisi dhidi Wamarekani weusi. Hata hivyo tangazo hilo halijazima ari ya waandamanaji kumiminika mabarabarani.

Kamatakamata nchini Marekani

Licha ya uwepo mkubwa wa askari polisi na maafisa wa Gadi ya Taifa katika mji wa Minneapolis, na licha ya kuanza utekelezwaji wa agizo la kutotoka nje kuanzia saa mbili usiku wa jana Jumamosi katika mji huo, lakini wakazi wake walipuuza yote hayo na kumiminika mabarabarani kwa wingi kushiriki maandamano hayo ya kulaani ubaguzi wa rangi.

Mmoja waandamanaji katika mji huo amesikika akisema "hatutaki kafyu, tunataka uadilifu." Waandamanaji hao wameapa kuendeleza maandamano yao hadi pale maafisa wote waliohusika na mauaji ya George Floyd watakapokatamwa na kufikishwa mbele ya sheria. Kufikia sasa ni askari mmoja tu kati ya wanne anayefahamika kama Derek Chauvin ambaye amekamatwa na kushtakiwa.

Ghasia Marekani kulaani mauaji ya Floyd (kulia)

Zaidi ya watu 200 wametiwa mbaroni katika jiji la New York pekee wakituhumia kuibua ghasia katika maandamano hayo.

Siku ya Jumatatu afisa mmoja mzungu wa jeshi la polisi la Marekani Derek Chauvin  alimuua kikatili George Floyd katika mji wa Minneapolis, ukatili ambao umezusha wimbi kubwa la maandamano na machafuko katika kona zote za Marekani.

Tags

Maoni