Jun 01, 2020 04:29 UTC
  • Upinzani wa Pakistan kuhusu ushindani wa silaha za nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan amesema kuwa, nchi yake inapinga ushindani wa silaha za nyuklia katika eneo hili.

Shah Mahmood Qureshi ameyasema hayo katika ujumbe alioutoa kwa mnasaba wa mwaka wa 22 wa kufanyika majaribio ya silaha za nyuklia ya Pakistan na kuongeza kwamba, lengo la Islamabad la kuwa na nguvu za nyuklia ni kwa ajili ya kujilinda na kudhamini usalama wake na wakati huo huo Pakistan inapinga aina yoyote ya ushindani wa silaha za nyuklia katika eneo hili. Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameongeza kwamba, Islamabad inaunga mkono usalama na amani ya kieneo na kimataifa na kwamba kama nchi yenye kumiliki silaha za nyuklia, itaendelea na mwenendo wake wa kuwa mvumilivu na kutekeleza vilivyo majukumu yake. Itakumbukwa kuwa tarehe 28 Mei 1998, na katika kujibu majaribio ya India ya silaha za nyuklia, Pakistan ilifanya majaribio kadhaa ya silaha hizo hatari. Pakistan na India zote zinamiliki vichwa vya nyuklia. Aidha nchi hizo mbili hazijatia saini Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia NPT.

Shah Mahmood Qureshi,  Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan

Matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ya kupinga ushindani wa silaha za nyuklia ni radiamali kwa siasa haribifu za Marekani katika eneo la kusini mwa Asia ambazo zimepelekea kushtadi ushindani wa silaha za nyuklia kati ya nchi za eneo hilo. Eneo la kusini mwa Asia limeathiriwa sana na ushindani wa silaha za nyuklia na silaha nyinginezo kati ya India na Pakistan unaotokana na sababu tofauti kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita. Tofauti za kugombania ardhi baina ya India na Pakistan zinaanzia tangu nchi mbili zilipogawanywa mwaka 1947 ambapo tayari zimeshapigana vita mara tatu katika kipindi cha nusu karne iliyopita. Ni baada ya hapo na ni katika kuinua uwezo wao wa kiistratijia na wa kijeshi ndio maana Pakistan na India zikajikita katika kustawisha elimu na teknolojia ya nyuklia hususan katika uga wa kijeshi. Kufanya majaribio ya makombora yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia, ni katika miradi ya kila mwaka ya nchi mbili hizo, jambo ambalo limezifanya Islamabad na New Delhi kuingia katika ushindani usio na kikomo ambao matokeo yake ni kuharibu tu vyanzo vyao vya kifedha na kiuchumi katika kugharamia zaidi mambo ya kijeshi kwenye hasa katika ushindani wao wa kuhodhi silaha za nyuklia.

India na Pakistan kila moja inamiliki silaha hatari za nyuklia

Hii ni katika hali ambayo, Taasisi ya Carnegie ya Usalama wa Kimataifa imetoa taarifa inayosema kuwa: "Pakistan inaharakia kustawisha uwezo wake wa nyuklia kutokana na wahka wake wa ushindani wa nyuklia na India." Ushindani wa silaha za nyuklia kati ya Pakistan na India ulimfanya Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2019 kutishia kuishambulia Pakistan kwa silaha za nyuklia. Mbali na sababu za ndani zinazoyafanya mataifa hayo kuzidisha ushindani wao wa nyuklia kwa muongo mmoja sasa, siasa chafu za za Marekani za kuzusha mifarakano katika kushadidisha mzozo baina ya Islamabad na New Delhi nazo zimechangia pakubwa na kupalilia moto wa ushindani wa nyuklia kati ya nchi hizo mbili. Kwa hakika siasa haribifu za White House katika kushadidisha mzozo kati ya India na Pakistan kupitia kuipendelea New Delhi na kuikandamiza Islamabad, ni katika ajenda za kigeni za Marekani zilizofikia kilele mwaka 2007 kupitia kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano wa kiistratijia wa nyuklia kati ya India na Marekani. Ni uchochezi huo wa Marekani ndio uliozisuku zaidi India na Pakistan katika ushindani wa silaha za nyuklia katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Tags

Maoni