Jun 01, 2020 07:12 UTC
  • Iyad na George, wahanga wawili wa ubaguzi wa Israel na Marekani

Matukio katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na Marekani yanaonyesha kilele cha ubaguzi katika utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani.

Jumamosi asubuhi, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walimuua shahidi kwa kumpiga risasi Iyad el-Hallak, kijana taahira Mpalestina aliyekuwa katika eneo la Babul Asbaat katika eneo la kale la mji wa Quds (Jerusalem). Katika upande wa pili nchini Marekani, George Floyd, raia mweusi mwenye asili ya Afrika Jumatatu iliyopita aliuawa kikatili na afisa wa polisi mzungu aliyetambuliwa kama Derek Chauvin katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota.

Matukio hayo yaliyojiri Israel na Marekani yana nukta nyingi za pamoja.

Kijana Mpalestina aliyeuawa shahidi na wanajeshi wa Israeli alikuwa na ulemavu wa kiakili, yaani mtu mwenye akili tahira. Jinai hii ya utawala wa Kizayuni ni misdaki ya wazi ya jinai dhidi ya binadamu na jinai ya kivita kwa mujibu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwani kijana aliyeuawa hakuwa na nafasi yoyote katika mapigano au vita na alikuwa na aina fulani ya ulemavu. Aidha mbali na hayo utawala wa Kizyauni wenyewe umekiri kuwa askari wake walimua shahidi kijana huyo mlemavu ambaye hakuwa na silaha yoyote. Kuhusiana na hili, Saeb Erekat  Katibu Mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) katika radiamali yake kufuatia kuuawa shahidi kijana huyo tahira Mpalestina mikononi mwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni ameitaka ICC ianzishe uchunguzi mara moja dhidi ya Israel.

Hali kama hivyo pia inashabihiana na kadhia ya George Floyd aliyeuawa kinyama huko Marekani. Raia huyo wa Marekani hakuwa mpiganaji na sababu pekee ambayo ilipelekea auawe na afisa wa polisi mzungu ni rangi ya ngozi yake, yaani mtu mweusi au mwenye asili ya Afrika. Nukta nyingine ni hii kuwa, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, utawala wa Kizayuni umewapa amri ya moja kwa moja askari wake wawaue Wapalestina kiholela. Nukta hiyo ni sawa na uungaji mkono rasmi wa Rais Donald Trump wa Marekani kwa mauaji ya George Floyd. Katika ujumbe kupitia Twitter, Trump alitoa vitisho kwa Meya wa Minneapolis na wakaazi wa mji huo kuwa atatuma Gadi ya Taifa mjini humo iwafyatulie risasi wakati wakiandamana kulaani mauaji ya Floyd.

Iyad el-Hallak aliyeuawa kinyama na askari wa utawala haramu wa Israel

Nukta nyingine ni kuwa kuuawa shahidi Iyad el-Hallak kumeibua maandamano makubwa ndani ya Palestina na hata katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, yaani Israel dhidi ya Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu. Nchini Marekani nako pia kumeshuhudiwa maandamano makubwa ya kitaifa kulaani mauaji ya George Floyd. Waandamanaji wenye hasira wamelaani vikali ubaguzi nchini humo. Baraza la mawaziri la Netanyahu limewapuuza waandamanaji na wakosoaji wa mauaji ya kijana tahira Mpalestina kama ambavyo naye Rais Trump amewataja wanaolalamikia mauaji ya Floyd kuwa ni magenge ya wahuni.

Tabia za Trump na Netanyahu zinaonyesha kuwa, kwa sasa fikra za ubaguzi wa rangi zinatawala na zimekita mizizi huko Israel na Marekani kuliko wakati mwingine wowote ule. Trump anawatazama wazungu kuwa kaumu bora zaidi kuliko kaumu zingine zote kama ambavyo Netanyahu anawatazama Mayahudi kuwa watu bora kuliko watu wengine.

George Floyd akiwa amekanyagwa na afisa wa plisi wa Marekani kabla ya kufariki papo hapo

Mauaji ya kijana Mpalestine mwenye ulemavu wa akili yameshangiliwa na Netanyahu na mawaziri wake kama ambavyo pia mauaji ya raia Mmarekani mwenye asili ya Afrika ni jambo la kuridhisha kwa Trump na wapambe wake.

Nukta nyingine ni kuwa, kuuawa shahidi  Iyad el-Hallak na George Floyd kumelaaniwa na walimwengu lakini kama ilivyo kawaida nchi za Ulaya zimenyamazia kimya mauaji hayo yaliyojiri Israel na Marekani na wala hazijaonyesha kukasirishwa na ubaguzi wa rangi katika maeneo hayo mawili.

 

Tags

Maoni