Jun 01, 2020 10:25 UTC
  • Maandamano ya kulaani ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi ya Marekani yasambaa duniani kote

Maandamano ya kulaani ubaguzi wa rangi na jinai ya polisi mweupe kumuuua Mmarekani mwenye asili ya Afrika sambamba na kuendelea kushuhudiwa katika miji na majimbo mbalimbali ya Marekani, lakini pia yamesambaa na kuenea kwa kasi katika nchi mbalimbali duniani hususan za Ulaya.

Maandamano hayo yameshuhudiwa katika mji mkuu wa Uingereza, London na mji mkuu wa Ujerumani, Berlin; ambapo mamia ya waandamanaji wamesikika wakipiga nara za "Hakuna amani iwapo hakuna uadilifu".

Baada ya kuandamana katika barabara za miji mikuu hiyo ya Uingereza na Ujerumani, waandamanaji hao wamefululiza hadi katika balozi za Marekani katika miji hiyo na kuwasilisha taarifa za kuonesha namna walivyochukizwa na ukatili huo wa polisi ya Marekani.

Kadhalika maandamano kama hayo yameshuhudiwa nje ya balozi za Marekani katika mji mkuu wa Ireland, Dublin na pia jijini  Auckland nchini New Zealand.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waandamanaji hao yalikuwa na jumbe zinazosema: "Haki kwa George Floyd", "Maisha ya Weusi yana Umuhimu", na "Siwezi Kupumua". Kauli hiyo ya "Siwezi kupumu" ilisikika ikitoka kinyonge kinywani mwa Mmarekani mwenye asili ya Afrika, George Floyd alipokuwa anauawa kikatili na polisi mweupe wa Marekani katika jimbo la Minnesota wiki iliyopita.

Maandamano ya kulaani ukatili wa polisi ya Marekani nchini New Zealand

Jumatatu iliyopita, afisa mmoja mzungu wa jeshi la polisi la Marekani kwa jina Derek Chauvin, alimuua kikatili George Floyd katika mji wa Minneapolis huku wenzake watatu wakitizama, ukatili ambao umezusha wimbi kubwa la maandamano na machafuko katika kona zote za Marekani.

Maandamano hayo yameshika kasi licha ya agizo la kutotoka nje nyakati za usiku katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo, na kamatakamata ya polisi.

Tags

Maoni