Jun 02, 2020 06:24 UTC
  • Trump asisitiza kuwakandamiza waandamanaji wanaolalamikia ubaguzi wa rangi nchini Marekani

Ubaguzi wa rangi na matumizi ya mabavu dhidi ya wale wanaotajwa kuwa watu wa rangi nchini Marekani na hasa weusi, ni jambo lenye historia ndefu nchini humo. Licha ya mapambano ya muda mrefu ya weusi kwa ajili ya kutetea haki zao, lakini wangali ni wahanga wakubwa wa ubaguzi na matumizi ya mabavu na hasa kutoka kwa polisi ya nchi hiyo.

Tukio la karibuni kabisa ni lile la mauaji ya kinyama yaliyotekelezwa taraehe 25 mwezi uliopita wa Mei katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota na polisi mweupe kwa jila la Derek Chauvin dhidi ya Mmarekani mweusi George Floyd, jambo ambalo limeibua maandamano makubwa ambayo yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa tena nchini Marekani, kwa lengo la kulaani ubaguzi wa rangi uliokita mizizi katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo. Polisi huyo mweupe alifanya kitendo cha kinyama kwa kubana shingo na kumyima pumzi taratibu Floyd, hadi alipoaga dunia, kwa kutumia goti la mguu wake wa kushoto, tena akiwa ametulia kabisa bila ya kuwa na wasiwasi wowote. Baada ya kukamatwa na kutuhumiwa kwa mauaji ya daraja ya tatu hapo tarehe 29 Mei, hatimaye Chauvin aliachiliwa huru kwa dhamana ya dola laki tano. Akilaani mauaji hayo ya kikatili yaliyofanywa na polisi dhidi ya Floyd, Seneta Kamala Harris, wa chama cha Democrat ambaye hivi karibuni pia alijaribu kugombea kiti cha rais wa Marekani alisema: Barabara za Marekani zimejaa damu ya watu weusi.

Licha ya kuwepo vitisho vya Rais Doland Trump na tahadhari za viongozi wa majimbo ya Marekani dhidi ya kufanyika maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo, lakini waandamanaji wenye hasira kali wangali wanaendelea na maandamano makubwa ya siku kadhaa sasa katika miji tofauti ya nchi hiyo kwa lengo la kulaani mauaji ya Floyd. Katika baadhi ya miji, waandamanaji wamekuwa wakikabiliana moja kwa moja na askari usalama na hata kupelekea hali ya hatari ya kutotoka nje kutangazwa katika miji 25.

Maandamano ya ghasia na uharibifu Marekani

Katika radiamali yake dhidi ya maandamano hayo ya kutetea haki za weusi na kulaani ubaguzi wa rangi na ambayo yamesababisha hasara kubwa ya mali nchini humo, Trump ametishia kutumia kila njia ikiwemo ya kijeshi kukandamiza wanaoshiriki maandamano hayo. Kuhusu suala hilo, Trump ambaye mwenyewe anatuhumiwa kuwa mchochezi mkuu wa ubaguzi dhidi ya watu wa rangi, amewataka mameya na magavama wa majimbo ya nchi hiyo kuchukua hatua kali dhidi ya waandamanaji na kuwataka watoe maombi ya kutumika wanajeshi katika kuwakandamiza waandamanaji. Trump anawatuhumu waandamanaji hao wanaopigania haki zao halali na kulaani ubaguzi wa rangi dhidi yao kuwa ni wahuni na waharibifu ambao wanaharibu mali za umma. Hivyo ametaka sheria kali zaidi zuchukuliwe dhidi yao na wapewe vifungo vya muda mrefu. Ametishia kwamba iwapo magavana hao hawatachukua hatua zinazofaa na kutekeleza matakwa yake, atalazimika kuingilia kati na kuamuru majeshi yatumie nguvu dhidi ya waandamanaji katika majimbo yanayoshuhudia ghasia. Kabla ya hapo Rais Trump pia alitangaza wazi, kupitia jumbe zake za Twitter, uungaji mkono wake kwa vitendo vya mabavu vinavyotekelezwa na gadi ya kitaifa dhidi ya waandamanaji katika mji wa Minneapolis, na kuongeza kuwa yuko tayari kutumia wanajeshi katika miji na majimbo yanayoshuhudia ghasia na machafuko nchini humo.

Kwa msingi huo Trump tayari amekwishatoa idhini na ishara ya kijani kwa polisi na askari usalama wa Marekani watumie nguvu na mabavu dhidi ya waandamanaji wanaofanya maandamano ya amani kulalamikia vitendo vya ubaguzi wa rangi dhidi yao. Ni wazi kuwa hatua hiyo bila shaka itavuruga utulivu na kuchochea zaidi ghasia pamoja na kusababisha hasara na maafa huko Marekani.

Trump hajatosheka na vitisho hivyo tu bali ametishia kwamba ataichukulia harakati ya ANTIFA Movement ambayo ndiyo inayoratibu maandamano ya sasa kuwa kundi la kigaidi. Wakati huohuo amelaani na kuvituhumu vyombo huru vya habari kwamba vinatumia uwezo wao wote kuwasha moto wa ghasia na chuki katika nchi hiyo.

Marekani hairuhusu hata waandishi habari kufanya kazi zao kwa uhuru

Madai hayo ya Trump yanatolewa katika hali ambayo rais huyo amekataa kabisa kulaani tukio la ubaguzi wa rangi la Charlottesville lililotokea mwaka 2017 ambapo wabaguzi weupe walihusika na mauaji. Katika radiamali yake kuhusu maandaano ya hivi karibuni ambayo yamepelekea watu 4100 kutiwa mbaroni, badala ya Trump kuonyesha masikitiko na kuomboleza na familia za wahanga pamoja na kutangaza hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahalifu wa vitendo vya mabavu katika jeshi la polisi na askari usalama, amekuwa akionyesha wazi wazi uungaji mkono wake kwa vitendo vya mabavu vya polisi hao dhidi ya watu wa rangi mbalimbali nchini Marekani. Jambo hilo limempelekea akosolewe sana ndani na nje ya nchi hiyo. Akikosoa hatua hiyo ya Trump dhidi ya wanaolalamikia vitendo vya ubaguzi wa rangi, Nancy Pelosi, Spika wa Kongresi ya Marekani amesema: Donald Trump hapasi kuchochea zaidi moto wa ghasia na machafuko kutokana na vitendo vyake. Rais wa nchi anapasa kuwa nembo ya umoja kati ya sauti tofauti na sio kuchochea mifarakano.

Pamoja na hayo, kuna uwezekano mdogo sana kwamba Trump huenda akabadilisha siasa zake za ubaguzi dhidi ya watu wanaolalamikia ubaguzi wa rangi, hivyo inatazamiwa kuwa vitendo vya ghasia na machafuko vitaendelea kuongezeka katika miji tofauti ya nchi hiyo katika siku zijazo. Jambo la kuzingatiwa hapa ni jinsi watu wa mataifa mengine wamekuwa wakifungamana na Wamareani wanaolalamikia ubaguzi na vitendo vya mabavu dhidi yao, kwa kuandaa maandamano na kulaani vitendo hivyo wanavyofanyiwa na serikali yao ya kibaguzi.

Tags

Maoni