Jun 02, 2020 07:42 UTC
  • Andrew Cuomo: Ghasia za mitaani nchini Marekani ndilo takwa la Trump

Gavana wa jimbo la New York nchini Marekani sambamba na kuunga mkono maandamano ya amani dhidi ya ubaguzi wa rangi ambao umekuwa ukiendelea nchini humo kwa mamia ya miaka, amesema kuwa, jumbe za Rais Donald Trump wa nchi hiyo zinabainisha wazi kwamba anapendelea ghasia zisambae na kuenea mitaani.

Andrew Cuomo ambaye ni gavana wa chama cha Democrat katika jimbo la New York ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari kuhusiana na hali ya virusi vya Corona jimboni humo ambapo akiashiria juu ya maandamano ambayo yameibua ghasia mjini New York na jumbe za Rais Donald Trump za kuwatuhumu waandamanaji kuwa ni majambazi, amesema kuwa, ghasia na machafuko ndilo takwa lake kuu.

Ukatili wa polisi wa Marekani dhidi ya Wamarekani weusi ni wa mamia ya miaka

Ameendelea kubainisha kwamba: "Tunashuhudia kuibiwa kwa harakati ya malalamiko." Gavana wa jimbo la New York amesisitiza hasira yake dhidi ya dhulma na kuongeza kwamba binafsi amesimama pamoja na waandamanaji. Andrew Cuomo ameendelea kufafanua kwamba kuna kesi 50 au zaidi zinazoshabihiana na kifo cha George Floyd dhidi ya Wamarekani weusi na kwamba chimbuko lake ni ubaguzi wa mamia ya miaka na dhulma, kama ambavyo pia amesisitiza kufanyika uchunguzi huru kuhusiana na polisi kutumia vibaya madaraka na uwezo wao.

Tags

Maoni