Jun 02, 2020 11:30 UTC
  • Mkuu wa Majeshi aonekana katika eneo la kukandamiza waandamanaji nchini Marekani

Muda mchache baada ya rais wa Marekani kutangaza serikali ya kijeshi na marufuku ya kutotoka nje, Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo Jenerali Mark Alexander Milley amekwenda kwenye maeneo ya kukandamiza waandamanaji kuona kwa karibu hali inavyoendelea na kazi inavyofanyika.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Jenerali Milley akisema kwenye mkanda mfupi wa video alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba kwa mujibu wa katiba ya Marekani, maandamano ya amani ni haki ya kila raia wa nchi hiyo.

Makumi ya maelfu ya Wamarekani jana usiku walishiriki kwa siku ya saba mfululizo katika maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi na mauaji ya George Floyd, raia wa Marekani mwenye asili ya Afrika aliyeuliwa kikatili na polisi mmoja mzungu katika mji wa Minneapolis, katika jimbo la Minnesota, licha ya rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza marufuku ya kutotoka nje nchi nzima na licha ya kutishia kuwapiga risasi waandamanaji.

Mkuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Mark Alexander Milley

 

Jumatatu ya wiki iliyopita, afisa mmoja mzungu wa jeshi la polisi la Marekani, anayejulikana kwa jina la Derek Chauvin, alimuua kikatili na kwa damu baridi kabisa, George Floyd Mmarekani mwenye asili ya Afrika katika mji wa Minneapolis huku wenzake watatu wakitizama na kuwazuia wapita njia wasimuokoa Mmarekani huyo. Ukatili huo umezusha wimbi kubwa la maandamano na machafuko katika kona zote za Marekani na sasa hivi Donald Trump ametangaza serikali ya kijeshi.

Machafuko hayo yamechochewa zaidi na matamshi ya kijuba, kibaguzi na ya jeuri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump wa Marekani ambaye amewaita wanaolalamikia ukatili huo kuwa ni 'vibaka,'  wahuni na majambazi.

Tags

Maoni