Jun 04, 2020 04:28 UTC
  • Guterres: Inasikitisha kuona ukatili kama huu katika nchi na mji mwenyeji wa ofisi za UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa inasikitisha kuona ukatili na machafuko ya sasa katika nchi na mji ambao ni makao makuu ya umoja huo.

Guterres ambaye alikuwa akiashiria machafuko makubwa na maandamano yanayofanyika katika miji na majimbo karibu yote ya Marekani kupinga ubaguzi wa rangi nchini humo baada ya mauaji yaliyofanywa na polisi dhidi ya Mmarekani mweusi, ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: "Nimesikitishwa na kuumizwa moyo kwa kuona ukatili unaofanyika katika mitaa ya nchi na mji wa New York ambao ni makao makuu Umoja wa Mataifa."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amechapicha bango lenye maandishi yanayosema: "Ubaguzi wa rangi ni chuki inayopaswa kupingwa na watu wote", na kuandika kuwa, vingozi wa Marekani wanapaswa kusikiliza malalamiko ya raia na upinzani na malalamiko yanapaswa kuelezwa kwa njia ya amani. 

Wapinzani wa ubaguzi wakiburutwa katika mitaa ya New York, Marekani

Awali Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet alikuwa tayari amelaani mauaji yaliyofanywa na polisi mzungu wa Marekani dhidi ya raia mweusi wa nchi hiyo na amewataka maafisa wa serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za haraka za kuzuia kukaririwa jinai kama hiyo. 

Miji mbalimbali ya Marekani hususan Minneapolis jimbo la Minnesota, imekuwa ulingo wa maandamano makubwa ya wananchi wanaopinga mienendo ya kibaguzi ya polisi wa nchi hiyo dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika. Machafuko hayo yalianza baada ya polisi mzungu, Derek Chauvin, akishirikiana na wenzake watatu kumuua kinyama George Floyd katika mji wa Minneapolis.

Machafuko hayo yamechochewa zaidi na matamshi ya kijuba, kibaguzi na ya jeuri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump ambaye amewaita wanaolalamikia ukatili huo kuwa ni vibaka, wahuni na majambazi. Watu wasiopungua 13 walikwua wameuawa kote Marekani hadi kufikia jana katika maandamano ya kulaani mauaji ya Floyd huku hali ikiendelea kuwa mbaya.

Utawala wa Marekani umelaaniwa kote duniani kwa kutumia mabavu kuwakandamiza waandamanaji wanaotetea haki.     

Maoni