Jun 04, 2020 07:55 UTC
  • Hata 'Mbwa Kichaa' akosoa mienendo ya Trump; zaidi ya 10,000 wakamatwa katika maandamano Marekani

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis maarufu kwa jina la "Mbwa Kichaa" ametangaza kuwaunga mkono wananchi wa Marekani wanaondamana kulaani ubaguzi wa rangi na mienendo ya kikatili ya polisi ya Marekani hususan dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Mattis alitangaza msimamo huo katika taarifa iliyochapishwa jana Jumatano na gazeti la The Atlantic, ambapo amemtuhumu Rais Donald Trump kuwa anajaribu kuwagawanya Wamarekani kimatabaka.

Ameeleza bayana kuwa, "Donald Trump ni rais wa kwanza katika uhai wangu ambaye hawaunganishi Wamarekani, bali hata hajifanyi kana kwamba anajaribu kuwaunganisha." Amesema taifa hili linashuhudia matokeo ya jitihada za makusudi za miaka mitatu za Trump za kuwagawa wananchi wa Marekani.

James Mattis amesema akiwatuhubu wananchi wa Marekani kuwa, "tunaweza kuungana bila yeye (Trump), hili si jambo jepesi, lakini linawezekana kwa ushirikiano."

Kamatakamata ya polisi ya US katika maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi

Kadhalika amekosoa hatua ya rais huyo kutumia jeshi la taifa kuzima maandamano ya kiraia, ambayo ni haki ya msingi iliyoanishwa kwenye katiba ya nchi hiyo.  Mattis ambaye ni jenerali mstaafu aliachia ngazi mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 2018, baada ya kuhitalifiana na Trump, na kujiunga katika orodha ndefu ya maafisa wa ngazi za juu serikali ya Trump ama waliojiengua wao wenyewe au kufukuzwa kazi.

Wananchi wa Marekani wamekuwa wakiandamana kwa zaidi ya wiki moja sasa, tangu alipouawa kinyama na polisi mweupe, George Floyd, Mmarekani mweusi katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota. Watu zaidi ya 10,000 wametiwa mbaroni katika majimbo mbalimbali ya Marekani kwa kushiriki maandamano hayo ya kupinga ubaguzi na dhulma.

Tags

Maoni