Jun 04, 2020 12:41 UTC
  • Wasiwasi wa Pentagon na hata Republican kwa hatua ya Trump ya kutumia wanajeshi kukandamiza waandamanaji Marekani

Maandamano makubwa ambayo hayajawahi kutokea mfano wake huko Marekani yamemtia kiwewe na kumuweka kwenye hali ngumu rais wa nchi hiyo mwenye majigambo na majivuno mengi, Donald Trump na kumfanya atoe amri ya kutumiwa jeshi, suala ambalo limelalamikiwa na Wizara ya Ulinzi, lakini hata wanachama wenzake ndani ya chama cha Republican nao hawakubaliani na uamuzi wake wa kutumia nguvu za kijeshi kukandamiza waandamanaji.

Hatua hiyo ya Trump imeifanya Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo Pentagon kuelezea wasiwasi wake na kusema haidhani kwamba ni kwa maslahi ya Marekani kutumiwa nguvu za kijeshi kwani hilo ni chaguo la mwisho kabisa kikatiba. Itakumbukwa kuwa tangu siku ya Jumatatu, Donald Trump alikuwa anatoa vitisho vya kutumia nguvu za kijeshi kwa madai ya kulinda mali na roho za Wamarekani. Jumatatu wiki hii alitishia kuwa atatumia sheria ya uasi iliyopasishwa mwaka 1807 ambayo inamruhusu rais wa Marekani kutumia wanajeshi kukandamiza machafuko na uasi wa kiraia. Katika hotuba yake ailiyoitoa siku hiyo, Trump aliwaambia wakuu wa majimbo ya Marekani kwamba:  Tunataka kumaliza machafuko haya kwa nguvu kubwa tena kubwa sana

Askari wa Marekani wakiwa wamemntia pingu Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika

 

Hatua hiyo ya Trump ya kutumia nguvu za kijeshi katika kukandamiza maandamano kwenye miji mbalimbali ya Marekani imelalamikiwa vikali na makamanda wa kijeshi na maafisa waandamizi wa Pentagon. Maafisa hao wanajaribu kumfahamisha Trump kwamba hakuna ushahidi makini wa kuonesha kuwa hali mbaya nchini Marekani imefikia hatua ya kutumiwa chaguo la mwisho kabisa la kulinda usalama wa nchi hiyo. Afisa mmoja wa Pentagon amesema, matumizi yoyote ya jeshi ni chaguo la chini na la mwisho kabisa katika kukabiliana na machafuko. Kwa kawaida wakuu wa majimbo ya Marekani huwa wanatumia Gadi ya Taifa, polisi, askari wa kulinda usalama na maafisa wa kiraia kukabiliana na maandamano ya upinzani. Hata hivyo ndani ya katiba ya Marekani kuna sheria ya uasi ya mwaka 1807 ambayo inamruhusu rais wa nchi kutuma wanajeshi kwenye majimbo ya nchi hiyo kukandamiza maandamano. 

Afisa mwingine mmoja wa masuala ya ulinzi ametumia sheria zinazowazuia wanajeshi kutumika katika utekelezaji wa masuala ya kiusalama ya ndani ya nchi na kuongeza kuwa, suala kubwa lililopo hivi sasa Marekani ni kutumiwa sheria za kieneo na za majimbo si kutumiwa wanajeshi. Hata baadhi ya maafisa wa Gadi ya Taifa hawakurishidhwa na kupewa kazi ya kurejesha utulivu katika jamii ya Marekani wakisema hiyo ni kazi ya jeshi la polisi na maafisa wengine wa kulinda usalama wa ndani ya nchi.

Donald Trump

 

Alaakullihaal, njama za Trump za kujaribu kukandamiza maandamano makubwa ambayo hayajawahi kutokea mfano wake katika historia ya hivi karibuni ya Marekani, zimelalamikiwa pia na wanachama wenzake ndani ya chama tawala cha Republican. Katika hatua ambayo ni nadra kutokea, wajumbe wa Baraza la Sanate la Marekani kutoka chama cha Trump mwenyewe yaani cha Repoublican nao wamemlaumu rais huyo kwa hatua anazochukua kukabiliana na waandamanaji. Malalamiko na ukosoaji huo wa maseneta wa chama cha Republicna umekuja siku moja baada ya jeshi la polisi la Marekani kutekeleza amri ya Trump ya kuwashambulia waandamanaji kwa gesi ya pilipili na hatua yake ya kwenda mbele ya kanisa moja karibu na White House kwa ajili ya kupigwa picha na waandishi wa habari.  Ben Sasse, seneta wa Marekani kutoka chama cha Republican cha Donald Trump amesema, moja ya haki za kimsingi kabisa katika katiba ya Marekani ni haki ya kuandamana na mimi ninapinga (kitendo cha Trump) cha kwenda kupiga picha na waandishi wa habari mbele ya kanisa na kutowajali watu wanaoandamana kwa amani. Maseneta wa chama cha Democrats pia wamekasirishwa sana na jinsi Trump anavyoamiliana na waandamanaji. Siku ya Jumanne, maseneta wa chama hicyo waliwasilisha muswada wa kulitaka Baraza la Sanate lilaani kitendo cha Trump cha kutoa amri ya kutumiwa risasi na gesi za kutoa machozi kuwatawanya watu wanaoandamana kwa amani. 

Kiujumla hali nchini Marekani ni mbaya sana zaidi ya watu wanavyofikiria. Hivi sasa Donald Trump mwenye majivuno na majigambo mengi, amelemewa na migogoro ya kiuchumi, kijamii, kiusalama, kiafya, wimbi la maambukizi ya corona na migogoro meingine mingi. Lakini badala ya kutumia busara, ndio kwanza rais huyo mwanagenzi wa Marekani anashindwa kudhibiti kiburi chake, anatoa amri kali za kukandamizwa kikatili na kijinai watu wanaoandamana kwa amani kiasi kwamba baadhi ya wanasiasa kama vile Mbunge Adam Schiff wa Marekani wamemuamua kuweka pembeni maneno ya kidiplomasia na wanamtaka waziwazi Trump afumbe 'domo' lake, aache kuchochea ghasia, na aachane na kiu yake ya kumwaga damu za watu wasio na hatia.

Tags

Maoni