Jun 27, 2020 06:58 UTC
  • Vikwazo vipya vya Marekani; kujitaabisha kusio na maana kwa lengo la kuidhoofisha Iran

Serikali ya Trump imekuwa ikifanya kila njia kupitia kampeni yake ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran ili kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu isalimu amri na kutekeleza matakwa yake haramu na yasiyo ya kisheria; na baada ya kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei 2018 ilianza kuiwekea Iran vikwazo vikali kabisa; na licha ya mwenendo huo kutokuwa na tija, lakini Washington ingali inashupalia kuendeleza vikwazo.

Katika muendelezo huo, siku ya Alkhamisi ya tarehe 25 Juni, Marekani iliiwekea Iran vikwazo vyengine vipya. Vikwazo hivyo vimeyalenga mashirika manane ya sekta ya feleji na aina nyingine za vyuma. Shirika la kimataifa la feleji la Sirjan, shirika la Iran la Markazi la makaa ya mawe na shirika la feleji la Matil ni miongoni mwa mashirika ya Iran yaliyowekewa vikwazo hivyo.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya fedha ya Marekani imesema, wizara hiyo imeyawekea vikwazo pia mashirika manne ya feleji, aluminiamu na chuma ambayo yanajishughulisha na utaalamu wa bidhaa za vyuma za Iran ikiwa na pamoja na shirika moja lenye makao yake Hong Kong ambalo liko chini ya shirika la feleji la Iran la Mobarake. Wizara ya Fedha ya Marekani imeijumuisha kwenye orodha yake ya vikwazo ofisi moja ya uwakilishi yenye makao yake Ujerumani na ofisi nyingine tatu zilizoko Imarati  kwa sababu ya kumilikiwa au kuendeshwa na shirika la feleji la Mobarake. Vikwazo hivyo vinatekelezwa kulingana na amri nambari 13871 ya utendaji, ambayo inaagiza sekta za chuma, feleji na aluminiamu za Iran ziwekewe vikwazo. Kabla ya hatua hiyo, shirika la feleji la Mobarake lilikuwa limeshawekwa kwenye orodha ya vikwazo vya Marekani tangu mwaka 2018. Shirika la feleji la Mobarake la Esfahan ndilo linalozalisha kwa wingi zaidi feleji katika maeneo ya Asia Magharibi na Afrika Kaskazini; na kwa mujibu wa ripoti za duru za Marekani linachangia asilimia moja ya pato halisi la taifa la Iran.

Kiwanda cha feleji cha Mobarake cha Esfahan

Washington inaituhumu Tehran kuwa inatumia faida inayopata kutoka kwa wazalishaji wake wa feleji  na ofisi zake za uwakilishi za mauzo zilizoko nje ya nchi kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya fedha ya hatua inazochukua kila pembe ya dunia. Akizungumzia vikwazo hivyo vipya, Waziri wa Fedha wa Marekani, Steven Mnuchin amedai: "Utawala wa Iran unatumia faida unayopata kwa wazalishaji wa feleji na ofisi za uwakilishi za mauzo nje ya nchi kwa ajili ya kugharimia kifedha hatua za kuvuruga uthabiti inazotekeleza kila pembe ya dunia. Marekani imekusudia kuhakikisha inazitenga sekta kuu za uchumi za Iran ili mapato yanayotokana na sekta hizo yatumiwe kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Iran." Washington inajifanya inashughulishwa na ustawi wa huduma za jamii wa wananchi wa Iran wakati vikwazo vikali zaidi kuwahi kushuhudiwa ilivyoiwekea Iran na mashinikizo ya kiuchumi yanayoshtadi kila uchao hayajawa na taathira nyingne isipokuwa kuzifanya ngumu zaidi hali za maisha za Wairani. Serikali ya Trump ina tamaa kwamba, kwa kutumia mkakati wa umasikini na uasi itaweza kuchochea manung'uniko na kuzusha fujo na machafuko ndani ya Iran.

Washington inadai kwamba, kuiwekea Iran vikwazo vikali zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia kupitia sera yake ya mashinikizo ya juu kabisa, kutaifanya Tehran isalimu amri na kutekeleza matakwa 12 ya Marekani yaliyotangazwa na Pompeo Mei 2018. Hata hivyo muqawama wa kupigiwa mfano ulioonyeshwa na wananchi wa Iran mbele ya vikwazo vya kidhalimu vya Marekani umeikatisha tamaa serikali ya Trump, ambayo katika hali ya kutapatapa iliamua kuanzisha chokochoko nyingine mpya, kama kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kwenye orodha ya makundi ya kigaidi, kumuua kigaidi aliyekuwa kamanda wa kikosi cha Quds cha IRGC, shahidi Qassem Soleimani na kuwawekea vikwazo viongozi wa ngazi za juu wa Iran. Si hayo tu, lakini kila baada ya muda, Washington imekuwa ikitumia visingizio tofauti kuyaweka kwenye orodha yake ya vikwazo mashirika na shakshia wengine wapya hususan wanaosaidia kuongeza nguvu za kiuchumi za Iran hasa kwa kuendeleza usafirishaji bidhaa nje ya nchi.

Image Caption

Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ameahidi kuwa, baada ya kujitoa katika JCPOA na kutekeleza sera ya mashinikizo ya juu kabisa ataweza, kwa mawazo yake, kuibana Iran ikubali kufanya mazungumzo na nchi yake ili kufikia kile anachoamini kuwa ni 'makubaliano mazuri zaidi'. Maafisa wa serikali ya Trump wamesikika mara kadhaa wakidai kwamba, sera ya mashinikizo ya juu kabisa imefanikiwa na kuwawezesha kuyafikia malengo waliyokusudia, hasa la kuusambaratisha uchumi wa Iran. Miongoni mwa waliodai hayo ni waziri wa mambo ya nje wa serikali hiyo Mike Pompeo ambaye siku ya Alkhamisi alisikika akisema, kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran imefanikiwa. Pompeo alisema: "Hapana shaka yoyote kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran imefanikiwa."

Hivi sasa zaidi ya miaka miwili imepita tangu kampeni ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran ilipoanza kutekelezwa, lakini Trump hajaweza kufikia lengo alilokusudia kuhusiana na Iran; na ndio maana anaandamwa na lawama na ukosoaji wa kila upande wa mirengo mbali mbali ndani ya Marekani, hasa wakati huu wa kukaribia uchaguzi wa urais wa nchi hiyo utakaofanyika mwezi Novemba. Wakosoaji wanamshutumu Trump kuwa ni mtu asiye na stratejia athirifu na inayoeleweka kuhusiana na Iran, ameshadidisha mivutano isiyo na sababu na Tehran na kuitenganisha Marekani na waitifaki wake. Lakini si hayo tu, kushadidishwa mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Iran wakati huu ambapo Tehran inakabiliwa na mripuko wa kirusi cha corona ulioikumba dunia nzima kunadhihirisha jinsi serikali ya Trump isivyojali wala kuyapa umuhimu wowote masuala ya kibinadamu. Ni kama alivyoeleza Jamal Zahran, profesa wa Mahusiano ya Kimataifa ya kwamba: Kuendelezwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran katika hali ya maambukizi ya corona nchini humo ni jinai dhidi ya binadamu.../

Tags