Jul 01, 2020 10:23 UTC
  • Vikwazo vipya vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Venezuela na jibu kali la Rais Maduro

Tangu mgogoro wa kisiasa wa Venezuela uliposhadidi, Umoja wa Ulaya umekuwa pamoja na Marekani dhidi ya Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo.

Baada ya Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela kujitangaza Januari 23 mwaka jana kuwa Rais wa muda wa nchi hiyo, Umoja wa Ulaya na akthari ya nchi wanachama wa umoja huo, zilitangaza himaya na uungaji mkono wao kwa mpinzani huyo na kuanza kutekeleza vikwazo dhidi ya Venezuela.

Katika hatua ya karibuni kabisa, Jumatatu ya juzi, Umoja wa Ulaya uliwaweka katika orodha ya vikwazo viongozi 11 wa Venezuela kwa kile kilichoelezwa kuwa ‘kudhoofisha demokrasia na utawala wa katiba’. Umoja wa Ulaya umedai kwamba, utaendeleza juhudi zake zenye lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za amani. Kuwekwa viongozi hao wapya 11 katika orodha ya vikwazo, kunaifanya idadi ya viongozi na maafisa wa nchi hiyo waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya hadi sasa kufikia 36. Umoja wa Ulaya ulianza kutekeleza vikwazo dhidi ya Venezuela mwaka 2017. Vikwazo hivyo vinajumuisha kupiga marufuku uuzaji silaha, kuzuiwa mali na kuwekewa marufuku ya kutosafiri viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Juan Guaido (kulia) kiongozi wa upinzani nchini Venezuela anayeungwa mkono na Marekani

Hatua hiyo ya chuki na uhasama ya Brussels imekabiliwa na majibu na radiamali kali ya Rais Nicolas Maduro. Rais Maduro alimpatia mjumbe wa Umoja wa Ulaya nchini humo muda wa masaa 72 awe ameondoka nchini humo. Aidha Rais Maduro amesema kuwa, ukoloni wa Ulaya kwa Venezuela sasa basi.

Matamshi hayo ya Rais Maduro ni ashirio la karne kadhaa za ukoloni wa Ulaya hususan Uhispania katika eneo la Amerika ya Latini ambao haukuwa na natija nyingine ghairi ya kupora utajiri mkubwa wa eneo hilo sambamba na  kuziangamiza kikatili kaumu na jamii za eneo hilo.

Hivi sasa pia madola ya Ulaya katika fremu ya ukoloni wao yameendelea kung’ang’ania kuingilia masuala ya ndani ya eneo hilo ikiwemo Venezuela kuanzia mwaka 1999 wakati hayati Hugo Chavez aliposhika hatamu za uongozi nchini Venezuela. Tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa ikishuhudia mapambano mtawalia dhidi ya ubeberu wa Marekani, ambapo madola hayo yametanguliza mbele siasa za kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Jorge Jesus Rodriguez, Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Venezuela tarehe 27 Juni mwaka huu alitangaza habari ya kuweko njama za pamoja kati ya ubalozi wa Uhispania mjini Caracas na Leopoldo Lopez mmoja wa viongozi wa upinzani za kutaka kuwaua na kuwateka nyara viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Lopez amejificha katika ubalozi wa Uhispania mjini Caracas tangu Mei mwaka jana baada ya kufeli jaribio la mapinduzi la Juan Guaido dhidi ya serikali ya Rais Nicolas Maduro.

Katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni, Umoja wa Ulaya umeendelea kuituhumu serikali halali ya Venezuela na kutoa wito wa kile unachokitaja kuwa, “kuhuishwa demokrasia” kupitia uchaguzi huru na wazi wa rais katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta. Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa, utawala wa Maduro umedhoofisha demokrasia na kulenga moja kwa moja utawala wa kisheria na haki za binadamu kutokana na hatua zake zisizokoma.

Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya Novemba mwaka jana waliongeza kwa mwaka mmoja mwingine muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Venezuela katika mkutano wao uliofanyika huko Brussels Ubelgiji na kupiga marufuku kuiuzia nchi hiyo zana ambazo zinaweza kutumika kuwakandamiza waandamanaji. Aidha waliongeza marufuku ya kutosafiri kwa viongozi na maafisa 25 wa Venezuela sambamba na kuzuia mali zao wakidaia kwamba, vikwazo hivyo vya Umoja wa Ulaya vinaweza kubadilika na kuondolewa na kwamba, haviwalengi wananchi wa kawaida wa nchi hiyo.

Marekani na washirika wake wa Ulaya wanapigania demokrasia na kufanyika uchaguzi nchini Venezuela katika hali ambayo, wamepuuza na kudharua kabisa matokeo ya uchaguzi wa nchi hiyo ya mwaka 2018 ambapo asilimia 68 ya wananchi wa Venezuela walimchagua Maduro kuwa Rais wa nchi hiyo. Inaonekana kuwa, demokrasia inayotakiwa na madola hayo sio ile inayoridhiwa  na wananchi wa Venezuela ambao walimchagua Nicolas Maduro kwa wingi wa kura.

Maandamano ya wananchi wa Venezuela ya kumuunga mkono Rais Nicolas Maduro

Hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuwa pamoja na Marekani katika kuishinikiza serikali ya mrengo wa kushoto ya Venezuela na Rais Maduro aliyechaguliwa kihalali, inakumbusha kuwa pamoja na Washington baadhi ya madola hayo hususan Ufaransa na Uingereza katika mgogoro wa Syria, hatua ambayo hatimaye ilikuwa ni fedheha kubwa ya kisiasa kwa madola hayo katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Hivi sasa madola ya Ulaya yamekuja na mkakati ulele kwa ajili ya Venezuela ambapo yamekataa kuitambua serikali halali ya Maduro na badala yake yanamtambua na kumuunga mkono kiongozi wa upinzani Juan Guaido sambamba na kukariri kuiwekea vikwazo serikali ya Caracas. Msimamo huu wa Umoja wa Ulaya sio tu kwamba, ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya Venezuela ambao ni haramu, bali hatua hiyo ni kinyume kabisa na irada na matakwa ya wananchi wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Hii ni kutokana na kuwa, Marekani na madola ya Ulaya yakiwa na lengo la kufikia matakwa yao yanafanya juhudi za kumuweka madarakani kwa nguvu Juan Guaido kupitia mashinikizo ya kiuchumi na hata ya kijeshi dhidi ya Venezuela na serikali ya Maduro. Hata hivyo hadi sasa njama hizo zimefeli na kugonga mwamba kutokana na uungaji mkono wa jeshi na wananchi wa Venezuela kwa Rais Nicolas Maduro.

Tags

Maoni