Jul 01, 2020 11:23 UTC
  • Sergei Vershinin
    Sergei Vershinin

Russia imekosoa mienendo inayokinzana ya nchi za Magharibi ya kuiwekea vikwazo vya uchumi Syria na wakati huo huo zinaitisha mkutano wa kukusanya misaada eti ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa nchi hiyo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Vershinin amesema katika mkutano wa wafadhili uliofanyika Brussels chini ya anwani ya Msaada kwa  Mustakbali wa Syria na Kanda ya Magharibi mwa Asia kwamba: Kuitisha mkutano wa wafadhili wa Brussels na madai ya kuwasaidia Wasyria havina faida yoyote wakati vikwazo vikali vya kiuchuumi vya Marekani na Umoja wa Ulaya vikiwalenga na kuwadhuru moja kwa moja wananchi wa nchi hiyo. 

Afsia huyo wa Russia amesema kuwa, Moscow inaunga mkono misaada ya kibinadamu kwa wananchi wote wa Syria bila ya suala hilo kufanywa kwa malengo ya kisiasa au misaada hiyo kuwekewa masharti.

Vershinin ameongeza kuwa inasikitisha kwamba, mwishoni mwa mwezi Mei kabla ya kuitisha mkutano wa wafadhili wa Brussels, Umoja wa Ulaya ulilipiga chenga Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kurefusha vikwazo haramu vya upande mmoja dhidi ya Syria. Ameongeza kuwa, mwanzoni mwa mwezi Aprili pia viongozi wa serikali ya Washington walichukua uamuzi kama huo.

Wakimbizi wa Syria

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 baada ya makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakisaidiwa na Marekani, Saudi Arabia, Israel na washirika wao kuvamia ardhi ya nchi hiyo kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serekani halali ya nchi hiyo na kubadili mlingano wa nguvu kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel. Mgogoro huo umewalazimisha mamilioni ya raia kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi na maelfu miongoni mwao wameuawa.    

Tags

Maoni