Jul 03, 2020 11:32 UTC
  • Lawama kali za Russia kwa azimio lililopendekezwa na Marekani la kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran

Ikiwa ni katika kuendeleza siasa zake za kukabiliana na nguvu za kiulinzi na kijeshi za Jamhuri ya Kiislamu zinazozidi kuongezeka siku hadi siku, serikali ya Donald Trump huko Marekani imeanzisha kampeni kubwa ya kimataifa ya kuzuia kufutwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa azimio hilo, vikwazo vya silaha dhidi ya Iran inabidi viondolewe ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka huu wa 2020. Sasa ili kuzuia kutekelezwa azimio hilo, serikali ya Marekani imependekeza azimio jipya la kuzuia kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran, azimio ambalo hata hivyo limepingwa vikali na nchi nyingine duniani zikiwemo Russia na China.

Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia  jana Alkhamisi tarehe 2 Julai, kwa mara nyingine tena alitangaza kuwa nchi yake inapinga muswada wa azimio la Marekani kwa Baraza la Usalama unaotaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, muswada huo una vipengee ambavyo havina uhusiano wowote na utatuzi wa masuala yanayohusiana na mradi wa nyuklia wa Iran. Zakharova amesema: Muswada wa pendekezo la Marekani kwa Baraza la Usalama kuhusu kuongezwa muda usio na kikomo kwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran umejaa vitu vinavyohudumia siasa za vikwazo vya kiwango cha juu vya Marekani dhidi ya Iran na kwamba muswada huo unazungumzia masuala ambayo hayana uhusiano wowote na utatuzi wa masuala yanayohusiana na mradi wa nyuklia wa Iran. Moscow imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba hakuna sababu yoyote ya kuiwekea Iran vikwazo vipya hasa wakati huu ambapo nchi mbalimbali zinafanya juhudi za kuyalinda makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA.

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Trump ameitoa Marekani kwenye mapatano hayo sasa anadai eti bado ni mwanachama

 

Kwa vile moja ya vipengee vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran baada ya miaka mitano ya kuanza utekelezaji wa azimio hilo, sasa Marekani imeamua kuongeza njama zake za kujaribu kuzuia utekelezaji wa kipengee hicho. Washington ilianzisha wimbi la vita vya kisaikolojia tangu katikati ya mwaka 2019 na hadi hivi sasa inaendelea kutoa madai yayo kwa yayo dhidi ya Iran. Viongozi wa Marekani hasa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo, mara zote wamekuwa wakidai kuwa, iwapo Iran itaondolewa vikwazo vya silaha basi kutazuka mashindano ya silaha katika eneo la Asia Magharibi. Si hayo tu, lakini nguvu za Iran na waitifaki wake katika eneo hilo zitazidi kuwa kubwa na usalama wa utawala wa Kizayuni wa Israel utaporomoka vibaya.

Katika hatua ya baadaye, serikali ya Trump ilianzisha kampeni za kuwashawishi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waungane na Marekani katika njama hizo. Azimio lililopendekezwa na Marekani kwa Baraza la Usalama linataka kupigwa marufuku miamala ya aina yoyote ile ya silaha na Iran huku viongozi wa White House wakisisitiza kuwa, marufuku hiyo inapaswa kuwa ya muda mrefu na ya kuendelea na kusitolewe mwanya wowote wa kuondolewa. Muswada huo wa azimio la Marekani pia unazitaka nchi za dunia ziwe zinazipekua meli za Iran katika maji ya kimataifa na kutaifishwa mali za nchi na pande zote zitakazoshirikiana na Iran. Juzi Jumatano, Mike Pompeo alisema, serikali ya Marekani haitaki vikwazo vya silaha dhidi ya Iran viwe vya muda mfupi.

Azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama lililopasisha mapatano ya JCPOA

 

Hata hivyo njama hizo za Marekani zimekumbwa na upinzani mkubwa hasa kutoka kwa madola mawili makubwa yenye nguvu duniani yaani Russia na China ambazo zinaamini kuwa, kupitishwa azimio hilo la Marekani ni sawa na kuuongezea nguvu ubeberu na jeuri za nchi hiyo duniani. Madola hayo yanaamini pia kwamba, kupasishwa azimio hilo la Marekani ni sawa na kusambaratika kikamilifu mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Tukija katika uwezekano wa kupasishwa azimio hilo pia tutaona kwamba uwezekano huo ni mdogo sana, na hata viongozi wa Marekani wanalitambua vyema jambo hilo. Ikumbukwe kuwa azimio lolote la Baraza la Usalama lazima lipate kura za ndio za wanachama wasiopungua 9 tena kusiwe na kura yoyote ya veto kutoka kwa mwanachama yeyote wa kudumu wa baraza hilo. Russia na China ambao ni wapinzani wakuu wa azimio hilo la Marekani wana kura ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ukweli ni kuwa, Marekani imetengwa vibaya kimataifa. Na ndio maana Rais Hassan Rouhani akasema kuwa hatua ya wanachama 15 wa Baraza la Usalama ya kuunga mkono kwa kauli moja makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na azimio nambari 2231 lililopasisha mapatano hayo katika kikao kilichofanyika tarehe 30 Juni, 2020 ni ushahidi mwingine wa kushindwa vibaya siasa za Marekani mbele ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags

Maoni