Jul 04, 2020 03:07 UTC
  • Maandamano ya kupinga ubaguzi Washington yabadilika na kuwa maandamano dhidi ya Israel

Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi yanayofanywa na wanachi wa Marekani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Washington jana yalibadilika na kuwa maandamano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Watu walioshiriki katika maandamano hayo ambayo yalianzia katika Kumbukumbu ya Lincoln (Lincoln Memorial) hadi jengo la Kongresi mjini Washington walipiga nara na kaulimbiu zinazosema: "Israel, tunajua kuwa unauua pia watoto wadogo."

Christian Tabash ambaye ni miongoni mwa wasimamizi wa maandamano hayo alisoma taarifa kwa washiriki akilaani jinai na uhalifu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina. 

Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulikuwa umepanga kwamba Jumatano ya tarehe Mosi Julai ungeanza kutekkeleza mpango wake haramu wa kupora na kuunganisha asilimia 30 ya ardhi za Ufukwe wa Magharibi na ardhi zingine za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Hata hivyo umelazimika kuakhirisha na kusogeza mbele tarehe ya utekelezaji wa mpango huo baada ya kushadidi mashinikizo ya upinzani ya Wapalestina na ya nchi mbalimbali duniani. Mpango huo ni sehemu ya mapendekezo ya Rais Donald Trump wa Marekani yaliyowekwa katika kile kinachodaiwa ni "Muamala wa Karne".

Wamarekani wamekuwa wakiandamana katika miji mbalimbali wakilaani mauaji yaliyofanywa na polisi mzungu wa nchi hiyo dhidi ya raia mweusi, George Floyd na vilevile ubaguzi wa rangi unaofanyika kwa mpangilio na utaratibu maalumu nchini humo.  

Tags

Maoni