Jul 04, 2020 07:50 UTC
  • Corona na udharura wa kufutwa vikwazo vya upande mmoja kwa ajili ya kulinda uhai wa wanadamu

Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, vikwazo vya upande mmoja vinadhoofisha uwezo wa nchi zinazolengwa kwa vikwazo hivyo katika mapambano yao dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona na vinapaswa kufutiliwa mbali.

Majid Takht-Ravanchi amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kujadili athari mbaya za maambukizi ya virusi vya corona kwamba: COVID-19 ni adui wa pamoja wa wanadamu wote, na njia pekee ya kukabiliana na ugonjwa huo ni mshikamano wa kivitendo na ushirikiano wa dunia; kwa sababu hiyo vikwazo vya aina yoyote vina madhara kwa walimwengu wote.

Wakati virusi vya corona na ugonjwa wa COVID-19 ulioanzia katika mji wa Wuhan ulipovuka mipaka ya China, hakuna mtu aliyedhania kuwa virusi hivo vingeathiri karibu maeneo yote ya dunia katika kipindi kifupi. Hapana shaka kuwa virusi vya corona ni changamoto kubwa kwa jamii ya kimataifa na mapambano dhidi ya changamoto hiyo yanawezekana tu kwa mshikamano na ushirikiano wa wanadamu wote.

Kasi ya maambukizi ya virusi vya corona duniani ambavyo tayari vimeathiri karibu watu milioni 11, inaonyesha kuwa, virusi vivyo havitambua mpaka wa nchi na vinalenga jamii yote ya mwanadamu. Katika mazingira kama haya, kuwepo kizuizi cha aina yoyote kama vikwazo vya upande mmoja, kunadhoofisha jitihada za kimataifa za kukabiliana na janga hilo na kuzifanya hata nchi zinazoweka vikwazo hivyo zikabiliwe na tatizo kubwa la virusi vya corona. 

Hii leo Marekani ya Donald Trump ambayo ndiyo inayoongoza dunia kwa kuwa na idadi kubwa ya waathirika wa corona na idadi kubwa zaidi ya watu waliouawa na virusi hivyo, imezidisha siasa zake za upande mmoja za mashinikizo sambamba na vikwazo dhidi ya baadhi ya baadhi ya nchi baada ya kuanza maambukizi ya virusi vya corona. 

Vikwazo hivyo vya Marekani vimekuwa na taathira hasi katika uwezo wa kiuchumi na kitiba za nchi mbalimbali wa kukabiliana na janga hilo. Iran ambayo kwa miaka mingi imekuwa chini ya vikwazo vya upande mmoja vya Marekani, haikuweza kutumia uwezo wake wote kwa ajili ya kukabilina na maambuki ya corona baada ya kuanza janga hilo lakini hii leo na kutokana na jitihada kubwa za jamii ya madaktari na wauguzi wake, inahesabiwa kuwa miongoni mwa nchi zenye mafanikio katika mapambano dhidi ya maambukizi ya corona.

Kutokana na kutojulikana vyema virusi vya corona ambavyo kila uchao vinadhihiri katika sura na dalili mpya, inaonekana kuwa, kuna udharura wa kuwepo ushirikiano na kubadilishana uzoefu na tajiriba ili kuimarisha mapambano ya janga hilo. Suala hilo linawezekana tu pale nchi za kibeberu zitakapoweka kando sera zao za kihasama na vikwazo vya upande mmoja. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu ya kimataifa katika kukabiliana na corona utawezekana pale nchi mbalimbali zitakapoweka kando siasa finyu kama hizo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Mousavi anasema kuhusiana na umuhimu wa kudumishwa mapambano ya dunia dhidi ya corona chini ya usimamizi wa Shirika la Afya Duniani kwamba: "WHO ina nafasi muhimu sana katika mapambano dhidi ya corona, japokuwa virusi vya sera za kujichukua maamuzi ya upande mmoja vinachafua hatua za pamoja za wanadamu katika uwanja huu.”

Vikwazo vya upande mmoja mbali na kuwa vinadhoofisha jitihada za kimataifa za kupambana na corona, lakini pia vinashirikiana na virusi hvyo katika kulenga watu wa kawaida hususan wagonjwa. Suala hili linaonyesha kuwa, vikwazo ni jambo lisilokubalika, kinyume cha sheria na la kikatili. Kwani kudhoofisha haki ya uhai wa wanadamu kupitia vikwazo kunakinzana waziwazi na haki za kimsingi za kiumbe huyo.

Tags

Maoni