Jul 04, 2020 07:59 UTC
  • Borrel asema JCPOA ni mafanikio ya kihistoria

Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya amesema binafsi anaitakidi kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni mafanikio makubwa ya kihistoria yatakayosaidia katika mchakato wa kuangamiza silaha hatari za nyuklia duniani.

Josep Borrell amesema hayo katika taarifa aliyoitoa jana Ijumaa akijibu barua ya Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliyomuandikia mapema hiyo jana.

Sehemu ya barua hiyo ya Borrel kwa Dakta Zarif imesema, "nimepokea leo barua (jana Ijumaa) kutoka Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akieleza kuhusu wasi wasi wa Iran juu ya hatua ya nchi tatu za Ulaya (Ujerumani, Ufaransa na Uingereza) ya kutaka kuanzisha mchakato wa kutatua hitilafu ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA (Dispute Resolution Mechanism), kama ilivyoanishwa kwenye kipengee cha 36 cha mapatano hayo."

Amesisitiza kuwa, utekelezwa wa mchakato huo unahitaji jitihada za pamoja na irada njema ya kisiasa ya pande zote husika, wakati huu ambapo mapatano hayo ya kimataifa yanaeelekea kuadhimisha miaka mitano tangu kupasishwa kwake.

Mwandiplomasia huyo wa ngazi za juu wa EU amefafanua kuwa, makubaliano ya JCPOA yana umuhimu mkubwa kwa amani na usalama wa eneo na dunia nzima kwa ujumla.

Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Josep Borrel ameeleza bayana kuwa: Kama tunataka JCPOA iendelee kuwa hai inatupasa kuhakikisha kwamba, Iran inafaidika na mkataba huo mkabala wa utekelezaji wake kikamilifu. 

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rosemary DiCarlo kutangaza baada ya kumalizika kikao cha Baraza la Usalama la UN kwamba mapatano ya JCPOA ndiyo njia bora zaidi ya kudhamini amani na kuendeleza kwa njia ya amani miradi ya nyuklia ya Iran licha ya changamoto zilizopo. 

Tags

Maoni