Jul 04, 2020 11:42 UTC
  • Biden: Trump anazidi kuisambaratisha jamii ya Marekani

Mgombea wa chama cha Democrats katika uchaguzi rais wa mwezi Novemba mwaka huu wa 2020 wa nchini Marekani amemshutumu vikali rais wa nchi hiyo Donald Trump akisema kuwa, anakwepa majukumu yake na anazidi kufanya uchochezi unaotishia kusambaratika jamii ya Marekani.

Joe Biden amesema, leo hii Marekani inahitajia mno umoja na mshikamano kwani inakabiliwa na tishio kubwa ambalo haitowezekana kukabiliana nalo kama hautakuwepo mshikamano wa kweli kati ya Wamarekani wa matabaka na rangi zote.

Amesema, inasikitisha kuona kuwa rais wa hivi sasa wa Marekani anakwepa kutekeleza majukumu yake na jambo hilo halikubaliki kabisa. Ikumbukwe kuwa waungaji mkono wakubwa wa rais wa hivi sasa wa Marekani, Donald Trump ni magenge ya Wazungu wabaguzi wa rangi.

Mgombea huyo wa urais kwa tiketi ya chama cha Democrats huko Marekani pia amesema, Trump na chama chake wanajiona kuwa wao wako juu ya sheria.

Joe Biden

 

Vile vile amesema, si tu serikali ya Marekani imeshindwa kuwapatia ajira watu waliomaliza masomo nchini humo, lakini pia karibu watu laki tisa wamepoteza kazi zao katika sekta za kieneo za elimu pekee kutokana na kwamba tangu yalipoanza maambukizi ya kirusi cha corona na serikali ya Trump kukata mno bajeti ya sekta ya elimu, sekta hiyo imeathirika vibaya, suala ambalo nalo halikubaliki hata kidogo.

Uchunguzi wa hivi karibuni wa maoni uliofanywa nchini Marekani unaonesha kuwa, uungaji mkono wa Joe Biden umeongezeka sana hasa baina ya wapiga kura ambao kabla ya hapo walikuwa hawana uhakika watampa nani kura zao katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu yaani mwezi Novemba 2020 nchini Marekani.

Maoni