Jul 05, 2020 00:17 UTC
  • Sisitizo la Borrell la kulindwa JCPOA na siasa za kindumakuwili za nchi za Ulaya

Umoja wa Ulaya na Troika ya bara hilo inayojumuisha nchi za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa, zilikuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Hata hivyo baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo, nchi hizo zilikuwa na mwenendo hasi na usiokubalika katika kutetea na kulinda makubaliano hayo na pia katika utekelezaaji wake.

Kwa sasa wakuu wa nchi za Ulaya wanafanya jitihada za kutetea utendaji wao hasi katika uwanja huo.

Katika mkondo huo Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell Ijumaa wiki hii alijibu barua ya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif akisema: Ameazimia kufanya jitihada zaidi za kulinda mapatano hayo ya nyuklia kwa kushirikiana na pande zote husika na vilevile jamii ya kimataifa. Taarifa iliyotolewa na Borrel imesema: "Katika kipindi hiki cha kukaribia mwaka wa tano tangu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yalipotiwa saini, ninatumia fursa hii kukumbusha umuhimu wa mapatano haya. JCPOA ni matunda ya kihistoria kwa ajili ya mfumo wa kimataifa wa kuzuia silaha za nyuklia na yanasaidia sana kuimarisha usalama na amani ya kikanda na kimataifa. Mimi nimeazimia kufanya jitihada za kulinda mapatano haya kwa kushirikiana na pande zote husika na jamii ya kimataifa." 

Josep Borrell

Madai haya ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya yanakinzana na utendaji wa taasisi hiyo na vilevile Troika ya Ulaya kuhusiana na makubaliano ya JCPOA. Nchi za Ulaya zimekuwa zikidai kuwa, zinataka makubaliano hayo yaendelee kulindwa kutokana na mchango wake muhimu katika kulinda usalama na amani ya kikanda na kimataifa. Nchi hizo ziliahidi kufanya jitihada kubwa za kulinda mapatano hayo. Hata hivyo Umoja wa Ulaya na Troika yake zimekataa kutekeleza ahadi hizo hususan utekelezaji wa mfumo maalumu wa mabadilishano ya kifedha na kibiashara na Iran maarufu kama INSTEX kutokana na mashinikizo ya Marekani na ukosefu wa azma na irada ya kutosha.

Tunapochunguza misimamo ya nchi za Ulaya baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA tunaona kuwa, nchi hizo zimefeli pakubwa katika utekelezaji wa ahadi na majukumu yao mkabala wa Iran. Inaonekana kuwa, kutotekelezwa kwa majukumu hayo ni aina fulani ya ushirikiano wa pande mbili za Bahari ya Antantiki (Ulaya na Marekani) ili mashinikizo ya kiwango cha juu ya serikali ya Trump yaweze kuwa na taathira zaidi kwa Iran na hatimaye kuilazimisha Tehran ikubaliane na matakwa 12 yaliyotolewa mwaka 2018 na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo.

Mike Pompeo

Kwa upande wake, Iran imekubali kutekeleza makubaliano hayo ya JCPOA kwa kutilia maanani maslahi yake ya kitaifa na ilitarajia kwamba, wanachama wa kundi la 4+1 hususan wale wa Ulaya, pia watatekeleza majukumu yao. Ni kutokana na hali hiyo ndipo Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Sayyid Abbas Mousavi akasema: "Tehran itachukua hatua zinazofaa mkabala wa ubeberu na mienendo isiyo ya kuwajibika na inazitaka nchi tatu za Ulaya zitayarishe mazingira mazuri ya utekekelezaji wa makubaliano hayo badala ya kufuata kibubusa sera za mashinikizo ya kiwango cha juu za Marekani."

Ukorofi huu wa nchi za Ulaya haukupita hivi hivi bila jibu mwafaka la Iran. Alkhamisi iliyopita Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran, Muhammad Javad Zarif alimwandikia barua Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya na mratibu wa makubaliano ya JCPOA na kutaja ukiukaji wa nchi za Ulaya wa vipengele kadhaa vya makubaliano hayo kwa mujibu wa kifungu nambari 36 cha JCPOA. Barua hiyo ya Zarif imesisitiza kuwa, uingiliaji wa aina yoyote katika ushirikiano wa sasa wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki unapingana na vipengee vya JCPOA na unaweza kuwa na taathira mbaya kwa ushirikiano huo.

Muhammad Javad Zarif

Kabla ya hapo pia Iran iliwasilisha malalamiko yake mara mbili kuhusiana na kutowajibika Marekani na nchi tatu za Ulaya mkabala wa makubaliano ya JCPOA na baada ya kushindwa kupatikana ufumbuzi iliamua kupunguza utekelezaji wake wa mapatano hayo kwa mujibu wa kifungu nambari 36 cha makubaliano hayo yenyewe.

Sasa mpira uko kwenye uwanja wa nchi za Ulaya ili badala ya kupayukapayuka na kutoa ahadi hewa, zichukue hatua za kivitendo na kuacha kushirikiana na Washington katika vikwazo vyake dhidi ya Iran.   

Tags

Maoni