Jul 06, 2020 02:27 UTC
  • Sisitizo la Russia la kutatuliwa hitilafu za JCPOA kupitia Kamisheni ya Pamoja

Licha ya Umoja wa Ulaya na Troika ya Ulaya kuahidi kutekeleza ahadi zao katika fremu ya mapatano ya JCPOA, lakini pande mbili hizo zimeshindwa kabisa kutekeleza ahadi hizo.

Jambo hilo limeipelekea Iran nayo kusimamisha katika hatua tano sehemu ya uwajibikaji wake katika mapatano hayo. Suala hilo lilizipelekea nchi za Ulaya tarehe 14 Januari kutaka kutekelezwa mchakato maalumu wa kutatuliwa hitilafu za pande mbili, huku Iran ikitaka kutotekelezwa mchakato huo kwa mujibu wa kipengee cha 36 cha mapatano hayo ya kimataifa kutokana na nchi za Ulaya kuvunja ahadi zao kwa Iran.

Katika uwanja huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia siku ya Jumamosi ilitoa taarifa ikisisitiza juu ya udharura wa kutatuliwa hitilafu zilizopo katika mapatano ya JCPOA kupitia Kamisheni ya Pamoja ya mapatano hayo. Mtazamo wa Moscow ni kwamba licha ya kuwepo hitilafu kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Troika ya Ulaya, hitilafu hizo zinapasa kutatuliwa kwa msingi wa malengo ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Wakati huohuo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeashiria kutorishishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hatua za hivi karibuni za nchi tatu za Ulaya yaani Ufaransa, Ujerumani na Uingereza dhidi yake.

Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia akitangaza msimamo wa nchi hiyo kuhusu JCPOA

Kufuatia hatua ya nchi tatu hizo za Uaya ya kuwasilisha azimio lililo dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA, na wakati huohuo kutotekeleza majukumu na ahadi zao kwa Iran kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Alkhamisi alimwandikia barua Joseph Borell, Mkuu wa Siasa za Kigeni wa Umoja wa Ulaya akimfahamisha kwa mara nyingine kutofungamana nchi za Ulaya na kipengee cha 36 cha mapatano ya JCPOA kuhusu kutatuliwa hitilafu kupitia Kamisheni ya Pamoja ya mapatano hayo.

Wakati huohuo Muhammad Jawad Zarif amesema kupitia ujumbe wa Twitter kwamba tokea wakati wa kuanza kutekelezwa mapatano ya JCPOA hadi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshatumia kwa uchahche mara sita mfumo maalumu wa JCPOA katika kutatua hitilafu zinazohusiana na ukiukaji wa mara kwa mara unaofanywa na Marekani na Troika ya Ulaya kuhusu mapatano hayo.

Suala hilo linathibitisha wazi kwamba kinyume na propaganda na madai yanayotolewa na nchi za Magharibi kuwa Iran inakiuka mapatano ya JCPOA ni nchi za Ulaya na Marekani ndizo zinazokanyaga mara kwa mara mapatano hayo ya kimataifa. Mfano wa wazi ni kwamba Iran ilitumia mara tatu mfumo huo maalumu wa utatuzi wa hitilafu wa JCPOA dhidi ya Marekani tarehe 16 Novemba 2016 na tarehe 10 Mei na 17 Juni 2018, kutokana na nchi hiyo kukiuka wazi mapatano ya JCPOA na vilevile mara 2 dhidi ya nchi hiyo na nchi tatu za Troika ya Ulaya tarehe 8 Novemba 2018 na tarehe 8 Mei 2019 kwa kukiuka mapatano hayo. Ilitumia kwa mara ya mwisho mfumo au mchakato huo wa utatuzi wa hitilafu dhidi ya Troika ya Ulaya tarehe 2 Julai mwaka huu.

Kikao cha Kamisheni ya Pamoja ya JCPOA mjini Vienna, Austria

Lengo kuu la Marekani kukiuka wazi mapatano hayo ni kutaka kuyavunja moja kwa moja. Lengo la nchi za Ulaya kutaka kuyavunja mapatano hayo ni kutokana na kushindwa kwao kutekeleza ahadi zao kwa Iran na hasa mfumo wa mabadilishao ya kibiashara ya kifedha mashuhuri kama INSTEX na pia ushirikiano wao na Marekani katika kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran, kama tuilivyoona zikifanya hivi karibuni kupitia azimio lao dhidi ya Iran katika Bodi ya Magavana ya IAEA.

Jambo hili linathibitisha wazi kwamba kinyume na zinavyodai nchi za Ulaya kwamba zinafungamana na kuheshimu mapatano ya JCPOA, zimekuwa zikiyatumia mapatano hayo kimaslahi tu na kuiacha Iran pekee itekeleze majukumu yake huku zikiwa zimesimama pembeni bila kufanya lolote kwa manufaa ya serikali ya Tehran. Ni wazi kuwa Iran nayo kamwe haitakubali kushinikizwa na kutekeleza majukumu yake bila ya pande nyingine husika kutekeleza majukumu yao.

Tags

Maoni