Jul 06, 2020 07:47 UTC
  • Trump ajifanya tena daktari bingwa wa corona; FDA yaja juu

Shirika la Chakula na Madawa la Marekani FDA limekosoa vikali matamshi mapya ya rais wa nchi hiyo, Donald Trump aliyedai kuwa asilimia 99 ya kesi za corona hazina hatari yoyote na kusema kuwa madai hayo si sahihi hata kidogo.

Shirika la habari la Associated Press limenukuu taarifa rasmi ya shirika hilo ikipinga madai ya Donald Trump aliyedai kuwa asilimia 99 ya kesi za COVID-19 hazina madhara yoyote kwa mwanadamu na kusema kuwa, matamshi hayo ya Trump (ni upayukaji na) hayana msingi.

Shirika hilo la Chakula na Madawa la Marekani aidha limetilia mkazo udharura kwa wananchi wa nchi hiyoi kuchunga protokali na miongozo yote ya watu wa afya na kwamba ni wajibu kwa kila mwananchi wa Marekani kutumia barakoa na kuchunga masafa baina yake na watu wengine.

Janga la corona ni kubwa Marekani, lakini rais wa nchi hiyo, Donald Trump asema corona haina madhara yoyote

 

Ikumbukwe kuwa Trump anapinga vikali maelekezo yote hayo ya madaktari ikiwa ni pamoja na kutumia barakoa na muda wote amekuwa akitembea maeneo tofauti bila ya kuvaa barakoa wala kuchunga masafa baina yake na watu wengine. Tarehe 4 Julai ambayo ni siku ya uhuru wa Marekani, Donald Trump alidai kuwa vipimo vilivyochukuliwa vya corona vimeonesha kuwa asilimia 99 ya kesi za ugonjwa wa COVID-19 hazina madhara hata chembe.

Huko nyuma pia Trump alijifanya pia daktari bingwa wa kutibu corona kwa kudai kuwa dawa ya malaria ya Hydroxychloroquine ni tiba mujarab ya corona, madai ambayo yalikosolewa vikali na madaktari nchini Marekani. Hata Shirika la Afya Duniani WHO limelazimika kuacha kuifanyia majaribio dawa ya kutibu malatia ya Hydroxychloroquine kutokana na kutowasaidia chochote wagonjwa wa corona.

Kama hiyo haitoshi, baada ya hapo, Trump aliwataka watu wanywe na wajidunge sanitaiza yaani vitakasaji vya corona, ili kujikinga na ugonjwa huo.  

Tags

Maoni