Jul 07, 2020 07:23 UTC
  • UN: Magaidi na wenye chuki wanatumia janga la corona kuendeleza ajenda zao

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema magenge ya kigaidi na makundi ya kibaguzi na yenye misimamo mikali yanatumia janga la kimataifa la corona kuendeleza ajenda zao hususan kupanda mbegu za chuki na uhasama katika jamii.

Antonio Guterres amesema ingawaje kwa sasa bado ni mapema kutathmini athari za janga la corona kwa ugaidi, lakini makundi ya kigaidi kama ISIS na al-Qaeda na vile vile magenge ya kibaguzi kama 'white supremacists' na 'unazi mamboleo' yanalitumia janga hili kuzusha mgawanyiko katika jamii ya mwanadamu, kuchochea migogoro na kupanda mbegu za chuki na uhasama.

Guterres alisema hayo jana Jumatatu wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Ugaidi na kuongeza kuwa, genge la kigaidi kama la ISIS (Daesh) ambalo lingali linadhibiti baadhi ya maeneo katika nchi za Iraq na Syria linajaribu kujiimarisha upya katika nchi mbili hizo za Kiarabu.

Katibu Mkuu wa UN ameeleza bayana kuwa, janga la corona limesababisha aina mpya ya ugaidi unaotishia amani na usalama wa dunia, kama vile ugaidi wa kiteknolojia, ugaidi wa kibaiolojia na hujuma za kimtandao.

Watu zaidi ya milioni 11 kote duniani wamembukizwa virusi vya corona

Kwa upande wake, Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya ameuambia mkutano huo uliofanyika kwa njia ya intaneti kuwa, kuna udharura wa kuwepo uelewa wa kimataifa kuhusu taathira za janga la corona katika vita dhidi ya ugaidi.

Amesema ingawaje mashambulizi ya kigaidi yamepungua katika baadhi ya maeneo ya dunia kutokana na janga la corona, lakini maeneo mengine yangali yanashuhudia hujuma za magenge ya kigaidi.

Tags

Maoni