Jul 07, 2020 10:55 UTC
  • Rais Bolsonaro wa Brazil
    Rais Bolsonaro wa Brazil

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amebainika kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 au corona.

Mtawala huyo mwenye utata wa Brazil amekuwa akipuuzilia mbali janga la COVID-19 akiutaja ugonjwa huo kuwa mafua tu yasiyokuwa na athari kubwa.

Wasiwasi ulitanda katika kona zote za Brazil baada ya rais wa nchi hiyo kuchukuliwa vipimo vya ugonjwa hatari wa COVID-19.

Mashirika mbalimbali yametangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Rais  Bolsonaro , 65,  amelazimika kukubali kuchukuliwa vipimo vya corona baada ya kuonekana na dalili za ugonjwa huo. Ikumbukwe kuwa, rais huyo anafanya ukaidi kama ule wa rais wa Marekani, Donald Trump hasa kuhusu corona. 

Akizungumza na waandishi habari baada ya vipimo hivyo kutangazwa, Rais Bolsonaro amesema hakuna sababu ya kuogopa na kwamba maisha yataendelea huku akisema ana matumaini kuhusu mustakabali wa Brazil.

Ikumbukwe pia kuwa, rais huyo wa Brazil amekuwa akijifananisha sana rais wa Marekani, Donald Trump na mwezi Aprili mwaka huu, alikataa kuchukua hatua za kitaifa za kukabiliana na maambukizi ya kirusi cha corona. Matokeo yake ni kwamba hivi sasa baada ya Marekani, Brazil ndiyo nchi yenye wagonjwa na vifo vingi zaidi vya wagonjwa wa COVID-19 duniani.

Uzembe na ukaidi wa Rais wa Brazil anajulikana kwa jina maarufu la Trump wa Brazil limeisababishia maafa makubwa nchi hiyo

 

Maambukizi ya corona yameenea katika kona zote za Brazil. Hivi sasa zaidi ya watu milioni moja na laki sita na 27 elfu wameambukizwa kirusi hicho nchini humo na zaidi ya watu 66 elfu wameshafariki dunia.

Moja ya sababu kuu za kuenea kwa kasi na kwa kiwango kikubwa ugonjwa wa COVID-19 nchini Brazil ni misimamo ya rais wa nchi hiyo ambaye ni maarufu kwa jina la Trump wa Brazil. Rais huyo analaumiwa kwa kudai kuwa ugonjwa wa corona ni ugonjwa mdogo tu wa mafua na kwa kupinga kuchukua hatua za maana za afya kama vile karantini na uchungaji wa masafa baina ya watu ili kukabiliana na corona.

Maoni