Jul 12, 2020 13:10 UTC
  • New York Times: Mapatano ya Iran na China ni pigo kubwa kwa Trump

Gazeti la New York Times limechapisha sehemu ya waraka wa mapatano ya ushirikiano wa Iran na China na kusema kuwa mapatano hayo ni pigo kubwa kwa sera dhidi ya Iran za Rais Donald Trump wa Marekani.

Gazeti hilo maarufu la Marekani limechapisha ripoti yenye anwani inayosema: "China na Iran zinazidi kukurubiana na zinasimama kidete mbele ya Marekani kwa kushirikiana kijeshi na kibiashara." Gazeti hilo limesema waraka wa 'mpango wa ushirikiano wa miaka 25 wa Iran na China ni hatua itakayopelekea kudhoofika jitihada zilizo dhidi ya Iran za utawala wa Donald Trump.

New York Times imeongeza kuwa, imeweza kupata utangulizi wa mapatano hayo na kuongeza kuwa, kwa mujibu wa mpango huo wa ushirikiano, mashirika ya China yatashiriki katika miradi ya pamoja na Iran ya kiuchumi, kijeshi, kielimu, utafiti katika uga wa silaha pamoja na mabadilishano ya habari za kiusalama kwa lengo la kukabiliana na ugaidi, biashara ya dawa za kulevya, uhalifu wa mpakani na usafirishaji haramu wa binadamu.

Gazeti la New York Times limeendelea kuandika kuwa, ushirikiano wa Iran na China utakuwa hatari kwa Marekani na kwamba ushirikiano huo pia ni pigo kubwa kwa sera za Trump dhidi ya Iran baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA  ya mwaka 2015.

Baraza la Mawaziri la Iran mnamo Juni 21 lilipasisha rasimu ya 'mpango wa miaka 25 ya ushirikiano wa Iran na China'.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imepewa jukumu la kufanya mazungumzo ya mwisho na China kuhusu mpango huo na kuhakikisha kuwa maslahi ya muda mrefu ya Iran yanazingatiwa kabla ya mapatano hayo kutiwa saini na nchi mbili.

Tags

Maoni