Jul 14, 2020 02:40 UTC
  • Kuporomoka husiano wa Marekani na Russia

Uhusiano wa Marekani na Russsia umekuwa na panda shuka nyingi katika kipindi cha baada ya Vita Baridi. Hata hivyo baada ya kujitokeza mgogoro wa Ukraine hapo mwaka 2014 uhusiano wa Moscow na Washington uliingia katika mporomoko mkubwa na sasa hitilafu kati ya pande hizo mbili zimepanuka zaidi na zaidi.

Mbali na kukabiliana na Moscow katika masuala ya kijeshi na kiusalama, Washington imezidisha pia mashinikizo dhidi ya Russia katika masuala mbalimbali ya kisiasa, kidiplomasia, kibiashara, kiuchumi na katika uga wa nishati.

Kwa upande wake Kremlin imetahadharisha kuhusiana na hali hiyo. Msemaji wa Rais wa Russia, Dmitry Peskov anasema kuhusiana na suala la kuporomoka kiwango cha uhusiano wa nchi hiyo na Marekani kwamba: "Uhusiano wa pande mbili uko katika hali mbaya sana na tunaweza kusema kuwa, haijawahi kushuhudiwa." Moscow inaamini kuwa, hali hii inatawala masuala yote yaliyozusha hitilafu kati ya pande hizo mbili. Peskov anasema kuwa, hali hii ya kuporomoko uhusiano wa Moscow na Washington si katika masuala ya pande mbili tu bali pia imeathiri nyanja nyingine yakiwemo majukumu ya nchi hizo mbili katika masuala ya kimataifa hususan yale yanayohusiana na udhibiti wa silaha na mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Dmitry Peskov

Afisa huyo wa Russia alikuwa akiashiria hatua za mara kwa mara za Rais Donald Trump za kuiondoa Marekani katika mikataba na makubaliano ya kudhibiti silaha, suala ambalo lina taathira mbaya katika usalama na amani ya kimataifa. Rais Vladimir Putin pia amezungumzia suala hilo la uhusiano wa Moscow na Washington na kusema: Uhusiano huo unaathiriwa na mwenendo wa kisiasa wa ndani ya Marekani.

Marekani na Russia zinahitilafiana sana katika masuala ya kikanda na kimataifa kama mgororo wa Ukraine, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, mgogoro wa nyuklia wa Peninsula ya Korea, mgogoro wa Syria na kadhia kubwa zaidi kama suala la udhibiti wa silaha na mfumo unaotakikana wa kimataifa. Maslahi yanayogongana ya madola hayo mawili yenye nguvu kubwa ya kijeshi katika mambo kama uwezo wao wa siaha za nyuklia na ushawishi wa pande hizo mbili katika maeneo ya Ulaya mashariki, magharibi mwa Asia na America ya Latini vimeifanya Washington iitambua Russia kuwa tishio kubwa zaidi la Marekani. Hata hivyo hatua hizi za uhasama za Washington dhidi ya Moscow hazikunyamaziwa kimya na Russia. Makabiliano ya pande hizo mbili yameshika kasi zaidi katika kipindi hiki cha sasa. Pande hizi mbili zinahitilafiana na kukabiliana sana katika masuala mengi ya kimataifa na jinsi ya kutatua migogoro mbalimbali. Mbali na mpambano wa Moscow na Washington katika eneo la Ulaya mashariki na Syria, sasa makabiliano hayo yamepanuka na kujumuisha eneo la America ya Latini hususan kuhusiana na kadhia ya Venezuela. Katika masuala ya usalama, hitilafu za pande mbili zimeongezeka na kufikia kiwango cha juu kabisa baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano na mikataba ya kudhibiti silaha za kistratijia.

Makabiliano baina ya Marekani na Russia yameongezeka

Baada ya Marekani kujiondoa kwenye mikataba ya kudhibiti silaha kama ule wa silaha za nyuklia za masafa ya kati INF kwa kifupi uliotiwa saini mwaka 1987 na hatua ya Washington ya kukataa kuanza mazungumzo ya kurefusha mkataba wa kupunguza silaha za nyuklia wa New START ambao muda wake unamalizika Februari mwaka 2011, Moscow imefikia natija kwamba, Washinton inafanya mikakati ya kupanua zaidi uwezo wake wa makombora na silaha za nyuklia. Kuhusiana na kadhia hii Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Russia, Sergei Ryabkov anasema: Moscow haiwezi tena kuwa na imani na Marekani na haiwezi kuitambua nchi hiyo kuwa ni mshirika wa kistratijia katika masuala ya usalama na amani ya kimataifa.

Ukweli ni kwamba, hatua na maamuzi ya Donald Trump ya kudharau mikataba ya kimataifa hususan katika masuala ya udhibiti wa silaha imezidisha mivutano baina ya Marekani na Russia. Hapana shaka kuwa kuendelea hali hii kutazidisha hali ya ukosefu wa amani katika medani ya kimataifa na kushadidisha mashindano ya silaha baina ya madola makubwa husuan katika upande wa silaha angamizi za nyuklia.  

Tags

Maoni