Aug 02, 2020 01:30 UTC
  • Vita baridi baina ya China na Marekani: Trump kupiga marufuku TikTok

Vita baridi baina ya China na Marekani vinaendelea kushika kasi ambapo katika hatua ya hivi karibuni kabisa, Rais Donald Tump wa Marekani ametangaza kwamba anapiga marufuku aplikesheni ya video maarufu ya TikTok inayomilikiwa na China nchini Marekani.

Trump amechukua hatua hiyo baada ya tetesi kusambaa kuhusu uwezekano wa serikali yake kuchukua hatua dhidi ya Tik Tok. Trump amenukuliwa na waandishi wa habari kwenye ndege ya Rais ya Air Force One akisema wataizuia aplikeshini hiyo nchini Marekani. Ameongeza kuwa anaweza kutumia mamlaka ya dharura ya kiuchumi ama amri ya rais kuizuia Tik Tok na kusisitiza kwamba anayo mamlaka na kuwa amri hiyo itasainiwa leo.

Mapema wiki hii serikali ya Trump ilitaka aplikesheni hiyo kupitiwa upya na tume ya uwekezaji wa nje nchini humo, CFIUS, huku kukiwa na wasiwasi kwamba China huenda inaitumia kuichunguza Marekani.

Rais Donald Trump wa Marekani

Maafisa wa usalama wa Marekani wanadai kwamba aplikesheni hiyo ya kampuni ya ByteDance ya China, inaweza kutumiwa kukusanya data binafsi za raia wa Marekani.

TikTok imekanusha madai kwamba inadhibitiwa au inashirikisha data zake na serikali ya China.

Aplikesheni hiyo ambayo imepata ushawishi kwa haraka ina watumiaji karibu milioni 80 kila mwezi nchini Marekani na marufuku hiyo itakuwa pigo kubwa kwa kampuni ya ByteDance.

Hivi karibuni, mivutano na mikwaruzano kati ya Marekani na China imeongezeka kutokana na sera za ubinafsi, ubabe na utumiaji mabavu za Washington.

Maoni